1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji wa Istanbul atajwa kuwa sugu

3 Januari 2017

Vyombo vya habari nchini Uturuki vimewanukuu wataalamu wa kiusalama wakisema kuwa mwanamume aliyesababisha vifo vya watu 39 na kujeruhiwa kwa takriban watu 70 mkesha wa mwaka mpya mjini Istanbul, ni muuwaji sugu.

https://p.dw.com/p/2VBtv
Türkei Blumen vor dem Reina Nachtclub in Istanbul
Picha: Reuters/Y. Karahan

Gazeti moja la kiingereza nchini humo lilimnukuu mtaalamu wa masuala ya kigaidi  Abdullah Agar akisema kuwa jinsi mshambuliaji huyo alivyotekeleza kitendo hicho cha ushambulizi inaonyesha kuwa ni muuaji na huenda ikawa ashawahi kuuwa kwa risasi kabla ya tukio hilo . 

Agar alinukuliwa akisema kuwa , mshambulaiji huyo ni mtaalamu aliyedhamiria, na katili asiye na huruma anayejuwa jinsi ya kupata matokeo…na  huenda alishawahi kutumia bunduki katika maeneo halisi ya vita . 

Vyombo vya habari nchini Uturuki pia vimeonyesha video ya "selfie" wanayosema ni ya mshambuliaji huyo. Video hiyo iliyoonyeshwa kupitia runinga nchini Uturuki hii leo, inaonyesha mshukiwa huyo wa ushambuliaji akijichukuwa video katika eneo la Taksim. Haikubainishwa mara moja iwapo video hiyo ilichukuliwa kabla au baada ya shambulizi hilo la mkesha wa mwaka mpya katika kilabu cha Reina.

Vyombo mbali mbali vya habari vimeripoti kuwa mwanamume huyo anaaminika kutoka katika taifa la Asia ya Kati. Kulingana na gazeti la Haber Turk, mwanamume huyo anaaminika kutoka katika kabila la Waislamu la walio wachache  la Uighur la China, na kwamba aliwasili mjini Konya nchini Uturuki pamoja na mkewe na watoto wake wawili.

Türkei Polizisten und Bürger vor dem Reina Nachtclub in Istanbul
Mwanamke mmoja aonyesha mshangao nje ya kilabu cha Rheina kilichoshambuliwa, IstanbulPicha: Reuters/Y. Karahan

Operesheni kuendelezwa nchini Syria

Huku msako huo ukiendelezwa, naibu waziri mkuu wa Uturuki amesema kuwa serikali yake itaendeleza operesheni nchini Syria dhidi ya kundi la wanamgambo wanaojiita dola la Kiislamu IS, baada ya kundi hilo kudai kuhusika na shambulizi hilo.

Wakati huo huo, wizara ya mashauri ya kigeni ya Umoja wa Falme za Kiarabu - UAE imewataka raia wake kuahirisha mipango yote ya kusafiri nchini Uturuki hadi watakaposhauriwa tena. Wakati hakuna raia yeyote kutoka katika nchi hiyo aliyeuawa katika shambulizi hilo ambapo  raia mmoja wa Kuwait na wengine saba kutoka Saudia Arabia ni miongoni mwa wahanga.

Hapo jana usiku, vitengo vya polisi vya kukabiliana na ugaidi vilitekeleza operesheni mjini Istanbul huku msako dhidi ya mshambuliaji huyo ukiendelezwa. 

Kulingana na shirika la habari la DHA, helikopta zilitumika na barabara kufungwa wakati wa operesheni hiyo lakini hakuna habari zozote zilizotolewa kuhusiana na kukamatwa kwa mshambuliaji huyo.

Awali shirika la habari linalomilikiwa na serikali la Anadolu lilisema kuwa washukiwa wanane walikuwa wamezuiliwa kuhusiana na shambulizi hilo lakini mshambuliaji huyo hakuwa miongoni mwao.

Mwandishi: Tatu Karema
Mhariri: Iddi Ssessanga