1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshauri wa zamani wa Trump Navarro aamriwa kuripoti gerezani

11 Machi 2024

Mshauri wa zamani wa Donald Trump Peter Navarro ameamriwa kuripoti gerezani kufikia Machi 19 mwaka 2024. Hii inaweza kumfanya kuwa afisa wa kwanza wa juu wa utawala wa Trump kufungwa kuhusiana na uchaguzi wa 2020

https://p.dw.com/p/4dPSv
Marekani Washington | Peter Navarro
Peter Navarro anatuhumiwa kuidharau kamati ya bunge la MarekaniPicha: Eric Baradat/AFP/Getty Images

Navarro, ambaye aliwahi kuwa mshauri wa biashara wa Trump, anatarajiwa Machi 19 kuanza kifungo chake cha miezi minne kwa kukaidi wito kamati ya Baraza la Wawakilishi la Marekani ambalo lilichunguza shambulio la Januari 6, 2021, dhidi ya bunge la Marekani.

Mawakili wa Navarro wameiomba mahakama ya shirikisho ya Washington, kusitisha hukumu hiyo wakati Navarro akikata rufaa dhidi ya hukumu yake. Timu yake ya utetezi imeashiria kuwa itaiomba Mahakama ya Juu ya Marekani kuingilia kati ikiwa ombi lake litakataliwa.

Marekani Washington | Donald Trump na Peter Navarro
Donald Trump akiwa na aliekuwa mshauri wake Peter Navarro.Picha: Tasos Katopodis/Getty Images

Navarro, 74, alipatikana na hatia ya kudharau bunge mara ya mwisho Septemba kwa kukataa kukabidhi nyaraka au kukaa  kwa mahojiano na kamati ya Bunge iliyokuwa inaongozwa na Wademokrasti iliyochunguza ghasia za jaribio lililoshindwa la wafuasi wa  Trump kubadili matokeo ya uchaguzi wa 2020. Alihuhukumiwa mwezi Januari.

Soma pia: Kamati ya Januari 6 yatoa ripoti inayoeleza njama ya Trump

Navarro, mkosoaji wa China ambaye pia alimshauri Trump juu mbinu za kukabiliana na janga la UVIKO, amedai Trump alitumia kanuni ya upendeleo wa kisheria kwa raia inayokinga baadhi ya rekodi za rais na mawasiliano kufichuliwa.

Hata hivyo Jaji wa shirikisho aligundua kuwa Trump hakuwa ametumia rasmi sheria hiyo.

Steve Bannon, aliewahi kuwa mpanga mikakati wa juu wa Trump, pia alihukumiwa kifungo cha miezi minne jela kwa kukaidi kudharau wito wa Kamati ya bunge, lakini jaji amemruhusu kusalia huru wakati akikata rufaa.

Chanzo: Reuters