1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshindi wa tuzo ya amani China Liu Xiaobo afariki dunia

Caro Robi
14 Julai 2017

Mshindi  wa tuzo ya amani ya Nobel wa China, Liu Xiaobo, amefariki dunia hapo jana baada ya kunyimwa ruhusa na serikali ya China kuondoka nchini humo ili kupokea matibabu katika nchi ya kigeni.

https://p.dw.com/p/2gVr1
China Liu Xiaobo, Aktivist 1995
Picha: Reuters/W. Burgess

Liu aliekuwa na umri wa miaka 61 na alikuwa akiugua saratani ya ini alikuwa akitumikia kifungo gerezani cha miaka 11 tangu mwaka 2009 kwa kosa la kile kilichotajwa kuwa ni kuchochea kupunguzwa nguvu za serikali baada ya kusaidia kuandika waraka wa ombi linalofahamika kama "Charter 08" linalotoa wito wa kufanyika mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini China.

Liu, alikuwa mshiriki maarufu katika maandamano ya kuunga mkono demokrasia yaliyofanywa katika uwanja wa Tiananmen mnamo mwaka wa 1989. 

China ilikataa Liu kwenda nje ya nchi

Mwezi uliopita, aliondolewa gerezani na kulazwa katika hospitali moja iliyoko mjini Shenyang baada ya saratani ya ini aliyokuwa akiugua kufikia hatua ya mwisho kabisa. Hospitali hiyo ya Shenyang imesema kuwa mwanaharakati huyo alifariki dunia baada ya viungo vyake vya figo na ini kuacha kufanya kazi.

Liu Xiaobo
Liu Xiaobo na mkewe Liu Xia hospitalini Picha: picture-alliance/AP

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa risala za rambi rambi kufuatia kifo cha mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel akimtaja kuwa mpiganiaji jasiri wa haki za kiraia na mtetezi wa uhuru wa kujieleza.

Kamishna mkuu wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al Hussein amesema jumuiya ya kutetea haki za binadamu China na kote duniani imempoteza shujaa aliyetetea na kudumisha haki za binadamu kwa njia ya amani na bila kusita aliyefungwa jela kwa kusimamia haki.

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker na wa baraza la Umoja huo Donald Tusk wanesema wamesikitishwa mno na kifo cha Liu na kutoa wito kwa serikali ya China kuiruhusu familia ya marehemu kumzika kwa njia wanayoitaka na kuruhisiwa kuomboleza kifo chake kwa amani.

Mwanaharakati wa China aliyeko uhamishoni Marekani Chen Guangcheng ameushutumu vikali utawala wa China.

China yashutumiwa na jumuiya ya kimataifa

Serikali za Ufaransa, Uingereza na Marekani zimetoa wito kwa China kuruhusu familia ya Liu kuwa huru. Mke wa marehemu Liu Xia anatumikia kifungo cha nyumbani.

Hong Kong | Trauer um  Liu Xiaobo
Watu wajitokeza kuweka maua kumkumbuka LiuPicha: picture-alliance/AP Photo/Kin Cheung

Mkuu wa kamati ya tuzo ya amani ya Nobel Beris Reiss Andersen amesema serikali ya China ndiyo inabeba dhamana kubwa ya kifo cha mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel aliyotunukiwa mwaka 2010 kwa kutetea haki za binadamu China.

Mataifa ya Magharibi yameishtumu China kwa kukataa kumruhusu Liu kutafuta matibabu katika nchi za kigeni na kuitaka nchi hiyo kulegeza vikwazo vyake vikali dhidi ya wakosoaji wa serikali.

Wizara ya mambo ya nje ya China imejibu shutuma hizo kwa kuzitaka nchi nyingine kutoingilia masuala ya ndani ya taifa hilo.

Msemaji wa wizara hiyo Geng Shuang amesema nchi nyingine zinapaswa kuheshimu uhuru wa China kujitawala kuambatana na sheria zake akiongeza Liu alikuwa mhalifu aliyehukumiwa ambaye baada ya kugundulika na maradhi, vituo vya afya vya China vilifanya kila juhudi kumtibu.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga