1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msikiti mwekundu wakombolewa

Oummilkheir11 Julai 2007

Wapakistan wanaunga mkono uamuzi wa serikali wa kuwatoa wanaharakati msikitini

https://p.dw.com/p/CHB9
Wahanga wa mashambulio ya Msikiti Mwekundu
Wahanga wa mashambulio ya Msikiti MwekunduPicha: AP

Vikosi vya Pakistan vinakamilisha operesheni ya kuukomboa msikiti mwekundi mjini Islamabad,opereshini zilizogharimu maisha ya mkuu wa waasi Imam Abdul Rashid Ghazi na wafuasi wake zaidi ya 50 na wanajeshi wanane.

Opereshini ya kuukomboa msikiti mwekundu,ngome ya wafuasi wa itikadi kali inakurubia kumalizika,lakini kuna masuala chungu nzima ambayo bado hayajapatiwa majibu.Haijulikani kwa mfano hadi dakika hii wanawake wangapi na watoto wameuliwa ndani ya Lal Masjid,seuze hasara jumla ya maisha iliyopatikana tangu vikosi vya usalama vilipouvamia msikiti huo jana alfajiri.

“Vyumba vya mwisho mwisho vya eneo hilo,yakiwemo makao makuu na makaazi ya Ghazi vinaendelea kutakaswa.Wafuasi wa itikadi kali walikua wakiishi humo humo pia.Lakini hatutakawia kumaliza” amesema msemaji wa jeshi jenerali Waheed Arshad .

“Katika opereshini kama hii panahitajika muda,majumba yamejengwa karivbu na karibu.Hata hivyo vikosi vya usalama vinaendelea nyema na shughuli zao za safisha safisha.”

Jenerali Arshad amesema ajuavyo yeye hakauna maiti za wanawake na watoto zilizogunduliwa.

Ghazi ameuwawa kufuatia mvua ya risasi zilizokua zikifyetuliwa na wafuasi wake aliokua amefuatana nao na wanajeshi wa serikali katika sehemu za chini za chuo cha Qoraani.

Miripuko ilisikika usiku kucha hadi alfajiri ya leo.Wanaharakati watatu wameuliwa kufuatia mapigano ya jana usiku-lakini hakuna ripoti za mashumbulio mengine kwa sasa.

Vikosi vya usalama vimeimarishwa katika eneo hilo ambako waandishi habari hawaruhsiwi kuingia na sheria ya kutotoka nje imetangazwa katika mtaa huo.

Licha ya hasara ya maisha iliyosababishwa na kuvamiwa msikiti mwekundu idadi kubwa ya wananchi wanaunga mkono uamuzi wa serikali wa kuuvamia msikiti huo.Bibi mmoja anasema:

“Kwavile mazungumzo yameshindwa,serikali haikua na njia nyengine isipokua kuuvamia msikiti mwekundu.Si jambo ambalo lingeweza kuepukwa.Na ndio maana limetokea.

Hata waziri mkuu wa zamani,mwanasiasa wa upande wa upinzani Benzir Bhutto anaunga mkono opereshini hiyo ,akijiuliza hata hivyo:

“Serikali imefanya vizuri kuwavamia wanamgambo.Lakini hofu zangu zilikua pale msikiti ulipozingirwa.Kwamba imam Ghazi na wafuasi wake wajenge msikiti mkubwa kama vile.Na hofu zaidi ni pale nnapojiuliza kwanini idara za upelelezi zimeshindwa kugundua kwamba makombora na silaha chungu nzima zimeingizwa kati kati ya mji mkuu?”

Hata vyombo vya habari vya Pakistan,kwa jumla vinaunga mkono opereshini ya jeshi dhidi ya msikiti mwekundu vikikumbusha hata hivyo “hilo ni funzo kwa serikali ambayo kwa muda mrefu imekua ikiwalinda wafuasi wa itikadi kali kwaajili ya masilahi yake.

Rais Pervez Musharaf anatazamiwa kulihutubia taifa kesho na kutangaza mkakati mpya dhidi ya magaidi.