1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msikiti watiwa moto katika mzozo Mashariki ya Kati

12 Novemba 2014

Walowezi wa Kiyahudi wameutia moto msikiti katika Ukingo wa Magharibi kwa kile kinachoonekana kuwa ni shambulio la kulipiza kisasi wakati mzozo kati ya Wapalestina na Israel ukizidi kutokota.

https://p.dw.com/p/1DljJ
Wapalestina wakipambana na vikosi vya Israel.
Wapalestina wakipambana na vikosi vya Israel.Picha: Coex/AFP/Getty Images

Machafuko hayo yaliokuweko kwa miezi kadhaa sasa yamepamba moto katika siku za hivi karibuni kwa kuenea kutoka Jerusalem ya mashariki hadi kwenye Ukingo wa magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel na katika maeneo ya jamii ya Waarabu nchini kote Israel na kuzusha hofu ya kuzuka kwa intifada mpya yaani uasi wa Kipalestina.

Katika hotuba ilionyeshwa na televisheni jana usiku Waziri Mkuu wa Israel Benjami Netanyahu amesema ameamuru kuchukuliwa kwa hatua kadhaa za usalama nchini kote kupambana na maandamano yanayozidi kuongezeka ya Waarabu walioko nchini humo.

Shambulio hilo la kuteketeza msikiti lililotokea alfajiri karibu na makaazi ya walowezi ya Kiyahudi ya Shilo, limekuja baada ya mashambulizi mawili tafauti hapo Jumatatu ambapo Wapalestina waliwapiga visu na kuwauwa mlowezi wa kike wa Kiyahudi kusini mwa Ukingo wa magharibi na mwanajeshi wa Israel mjini Tel Aviv.

Mashambulizi ya kisasi

Afisa wa usalama amesema walowezi waliteketeza kabisa ghorofa ya chini ya msikiti huo katika kijiji cha Al-Mugheyr karibu na mji wa Ramallah ulioko Ukingo wa magharibi na polisi imethibitisha kuwepo kwa tukio hilo ambapo tayari imeanzisha uchunguzi.

Wanajeshi wa Israel katika makabiliano na Wapalestina.
Wanajeshi wa Israel katika makabiliano na Wapalestina.Picha: Reuters/Ammar Awad

Pia wakati wa usiku bomu la petroli limerushwa kwenye sinagogi la kale ambalo halitumiki kwa ibada katika mji wanakoishi Waisraeli-Wakiarabu wa Shfram.

Shambulio dhidi ya msikiti linakuja wakati ghadhabu ya Wapalestina ikitokota kutokana na vikosi vya Israel kumuuwa kwa kumpiga risasi muandamanaji wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 22 kusini mwa Ukingo wa magharibi hapo Jumanne.

Juhudi za kuzima mzozo

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameelekea nchi jirani ya Jordan kwa mazungumzo na Mfalme Abdulla ambayo yanatarajiwa kulenga hali ya machafuko hayo inayozidi kuwa pamoja na mashambulizi yanayoongozwa na Marekani didi ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria.

Waarabu wa Kiisrael katika maandamano dhidi ya serikali.
Waarabu wa Kiisrael katika maandamano dhidi ya serikali.Picha: Ahmad Gharablia/AFP/Getty Images

Jordan ambayo dhima yake ni mlezi wa maeneo takatifu ya Waislamu yalioko Jerusalem ya mashariki kama ilivyotajwa katika mkataba wa amani wa mwaka 1994 na Israel, imeelezea wasi wasi wake juu ya hatua ilizochukuwa Israel katika eneo takatifu la msikiti wa Al Aqsa lililozusha mapambano.

Kampeni ya makundi ya Kiyahudi ya sera kali za mrengo wa kulia ya kutaka kupatiwa haki ya kufanya ibada ndani ya eneo hilo ambalo ni mojawapo ya maeneo nyeti kabisa Mashariki ya Kati imechochea mvutano ambao tayari ulikuwa mkubwa kwa sababu ya kutanuliwa kwa makaazi ya walowezi ya Kiyahudi katika eneo la Jerusalem ya mashariki lililotwaliwa na Israel.

Mwandishi:Mohamed Dahman,ap,afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman