1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msimamo wa Marekani kwa Ukraine

13 Desemba 2013

Marekani imeonyesha msimamo wake kuhusu Ukraine kwa kuivutia nchi hiyo iliyokuwa moja ya nchi za Jamhuri ya Kisovieti, kuelekea katika umoja wa nchi za Ulaya na kujiondoa kwenye uhusiano na Urusi.

https://p.dw.com/p/1AZUt
Waandamanaji mjini Kiev-Ukraine
Waandamanaji mjini Kiev-UkrainePicha: Reuters

Hivi karibuni Marekani imeimarisha msimamo wake kwa kulaani namna polisi inavyowatendea waandamanaji na huku afisa wake wa kibalozi wa ngazi za juu akijitokeza kwenye uwanja wa maandamano na kuzungumza na waandamanaji, mjini Kiev.

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, alimpigia simu rais wa Ukraine, Viktor Yanukovych na kumweleza wasiwasi wake na kuonesha kwamba Marekani inafikiria hata kuweka vikwazo dhidi ya Ukraine.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanajiuliza kwa nini Marekani imekuwa na shauku ya kujiingiza kwa undani katika masuala ya Ukraine, wakati tayari Rais Yanukovich keshafanya uamuzi wa kutosaini mkataba wa kujiunga na umoja wa Ulaya ambapo mataifa mengi ya magharibi yameshaona hakuna jipya kutoka kwa Ukraine katika mkataba huo.

Mwelekeo wa baadae wa Ukraine

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa, mwelekeo wa Ukraine kwa baadae, ni mwendelezo wa harakati za kiitikadi za miongo kadhaa. Mmoja wa viongozi wa halmashauri ya masuala ya kigeni, Charles Kupchan, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, tangu wakati wa kumalizika kwa vita baridi kati ya marekani na Urusi, Marekani na washirika wake wa nchi za Ulaya, wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuzivutia upande wao nchi zilizokuwa sehemu ya Muungano wa Kisovieti, na mojawapo ya vivutio ni kutoa misaada hasa ya kiuchumi kiasi kwamba takwimu zinaonyesha kuwa nchi zote za Ulaya zinazojiunga na umoja wa NATO pamoja na Umoja wa Ulaya, zina maendeleo kuliko ambazo bado hazijajiunga.

Pamoja na kuwa nchi za kitovu cha ulaya zimekwisha onyesha mwelekeo wake kuhusu kujiunga na umaoja wa ulaya, lakini Rais wa Urusi Vladimir Putin anataka kutengeneza umoja wa nchi zilizokuwa za kisovieti kutokana na kuwa na desturi zinazofanana.

Kupchan ameliambia pia shirika la habari la AFP kuwa, mpaka sasa wanashuhudia jitihada za Rais Putin kuivutia Ukraine upande wa Urusi, huku Marekani na washirika wake wa nchi za ulaya wanaivutia ukraine upande wao.

Polisi wa Ukraine katika kuzuia maandamano
Polisi wa Ukraine katika kuzuia maandamanoPicha: DW/ A. Savitski

Vuta nikuvute

Katika vuta nikuvute hiyo, Umoja wa Ulaya umesema kuwa hautasaini mkataba wa biashara huria na Ukraine, iwapo nchi hiyo itaamua kujiunga na umoja wa nchi zilizokuwa za Kisovieti, na wakati huo huo Urusi imeitishia Ukraine kuwa itawapandishia bei ya gesi na kuwakazia masharti ya kibiashara, iwapo nchi hiyo itaamua kujiunga na jumuiya ya umoja wa ulaya kwa kivutio cha pesa.

Kutokana na msimamo huo wa Urusi, aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Ukraine Steven Pifer anasema kuwa, Urusi inailazimisha Ukraine kufanya uamuzi wa ama kujiunga na umoja wa nchi za kisoviet au umoja wa Ulaya na kukubali kukaziwa masharti ya kibiashara na Urusi, na mwanadiplomasia huyo kaongeza kuwa, kupunguza makali ya mizozo ya kisiasa inayoendelea Ukraine haitafaa kitu iwapo bado kuna mvutano kati ya Marekani na Urusi, ambapo vurugu za Ukraine zinaipa urusi upenyo mkubwa zaidi kwa nchi hiyo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani,John Kerry, wiki iliyopita alipokuwa akiendelea na ziara yake huko Moldova, alisisitiza kuwa nchi za umoja wa ulaya haupo katika ushindani kutokana na kile kinachoendelea Ukraine

Jumatano wiki hii, waziri mkuu wa Ukraine, Mykola Azarov, alisema kuwa nchi yake itahitaji mkopo wa kiasi cha EURO bilioni 27.5, kabla ya kusaini mkataba na nchi za umoja wa ulaya, ambapo katika hizo pesa kiasi cha EURO bilioni 2 nchi hiyo itaweza kuilipa kampuni ya gesi ya urusi GAZPROM.

Hili ni jumba la Ikulu ya Marekani mjini Washington
Hili ni jumba la Ikulu ya Marekani mjini WashingtonPicha: Win McNamee/Getty Images

Marekani inaendelea kuwatia kishindo Ukraine, kwa kuishawishi nchi hiyo kujiunga na umoja wa ulaya, na kuiahidi kuisaidia kupata nafasi mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani, IMF

Mwandishi:Diana Kago/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef