1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga: kinyang'anyiro kitakuwa kikali

17 Agosti 2015

Msimu mpya wa ligi kuu ya kandanda Ujerumani ilianza mwishoni mwa wiki, huku timu zote zinazowania ubingwa zikipata ushindi. Katika benchi la ufundi, kulikuwa na meneja mpya. Thomas Tuchel

https://p.dw.com/p/1GGkk
Fußball Bundesliga 1. Spieltag Borussia Dortmund - Borussia Mönchengladbach
Picha: Getty Images/Bongarts/D. Grombkowski

Huku akitembea tembea pembeni ya uwanja wa Signal Iduna Park, ndani ya uwanja mambo yalionekana kuwa yale yale, ambapo Dortmund waliwakimbiza mchaka mchaka wapinzani wao Borussia Moenchengladbach. Na baada ya wachezaji Marco Reus, Pierre-Emerick Aubameyang na Henrikh Mkhitaryan ili kuipa Dortmund ushindi wa nne bila, kocha wa Gladbach Lucien Favre alisalimu amri na kusema kuwa BVB walikuwa timu bora kuwaliko na walistahili ushindi na pointi tatu. Marco Reus mmoja wa wafungaji wa Dortmund alisema walionyesha ari kubwa. "Tulitaka kuanza kwa kiwango cha juu. Tulijua kuwa Gladbach ina timu imara, inayocheza vizuri kiufundi, yenye kufanya mashambulizi ya kasi. Tuliumilki sana mpira, na nadhani tulisubiri wakati mwafaka, kisha tukacheza kwa kasi ubavuni. Nadhani tulifaulu katika hilo na ndio maana tukapata magoli hayo".

Fußball Bundesliga 1. Spieltag Borussia Dortmund - Borussia Mönchengladbach Trainer Lucien Favre
Thomas Tuchel ameanza msimu kwa ushindiPicha: picture-alliance/dpa

Bayer Leverkusen ilianza kampeni yao dhidi ya Hoffenheim kwa kupata ushindi wa mbili moja isipokuwa haikuwa kazi rahisi. Katika mchuano mwingine, Schalke waliwafunga Werder Bremen tatu bila.

Wengi hata hivyo walitaka kujua namna zitakavyoanza timu mbili zilizopandishwa daraja msimu huu na kutokana na matokeo ya jana, ni wazi kuwa Ingolstadt na Darmstadt hazijajiunga na Bundesliga kuwa watalii tu.

Darmstadt walicheza ugenini nyumbani kwa Hannover na kulazimisha sare ya mbili mbili, wakati nao vijana wa Ingolstadt wakipata ushindi wa moja bila dhidi ya Mainz katika mchuano wao wa kwanza kabisa wa Bundesliga. Kocha Ralph Hassenhüttl alielezea furaha yake "Nina furaha kubwa sana. Nikama kupatwa na wazimu kwa furaha. Hii ni hisia isiyoelezeka. Nadhani tulistahili kushinda. Lakini hata kama tungeshibda bila kustahili nisingejali pia. Lakini leo nadhani tulikuwa imara kabisa. Tulichea namna tulivyopanga na kufanya kila kitu sahihi kabisa".

Mpambano kati ya Augbsurg na Hertha Berlin ulikuwa wa mabavu ambapo penalti iliyofungwa na Salomon Kalou iliwapa vijana wa Berlin ushindi wa moja bila. Hapo jana, Wolfsburg ilibwaga Eintracht Frankfurt mbili moja. Huyu hapa Bas Dost aliyeifungia Wolfsburg bao la pili "Bila shaka nina furaha kuwa tumeshinda. Pia nimeona kuwa tunaweza kucheza vyema zaidi na hilo ni jambo zuri. Dhidi ya Frankfurt, tulitoka sare msimu uliopita mara mbili hivyo tulijua utakuwa mchuano mgumu. Leo tumeshinda. Lakini nadhani tunaweza kucheza hata vizuri zaidi na hilo ni jambo la maana".

FC Cologne walikamilisha wikendi ya kwanza ya michuano ya ufunguzi wa msimu kwa kuwafunga Stuttgart tatu moja

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga