1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msukosuko wa masoko ya fedha

19 Septemba 2008

Nafuu tena katika masoko ya fedha baada ya hatua za serikali ya Marekani na Uingereza.

https://p.dw.com/p/FLIT

Serikali na Bunge la Marekani-Congress wanakutana pamoja mwishoni mwa wiki hii kusaka njia za kufumbua kitandawili kilichoyakumba masoko ya fedha na msukosuko wa mabenki yake yanayotoa mikopo ya wanunuzi wa majumba.

Banki kuu ya Ulaya-European Central Bank imetangaza nayo hii leo tender ya dala bilioni 40 ili kutia jeki mfuko wa fedha taslim katika masoko kwa ushirikiano na banki kuu nyengine.Hata Ulaya masoko ya hisa yameanza kupata nafuu tena.

►◄

Mabenki na masoko ya hisa yameanza kufufuka i leo baada ya hatua za kuyatia jeki kuchukuliwa. Hatua ya jana iliochukuliwa na serikali ya Marekani mjini Washington na uamuzi wa serikali ya Uingereza mjini London kuzuwia uuzaji mfupi wa akiba za mabanki kumeleta nafuu haraka .

Hisa barani Asia nazo zimepanda thamani l baada ya zile za Marekani kutia faida nono kabisa isiowahi kuonekana tangu miaka 6 iliopita.Hii ikaongoza kupanda kwa thamani ya sarafu ya dala na wakati huo huo kupandisha zaidi bei ya mafuta ya petroli masokoni.Bei ya dhahabu lakini ilishuka.

Waziri wa hazina wa Marekani Henry Paulson na Mwenyekiti wa Bodi ya hazina Ben Bernanke , wanakutana mwishoni mwa wiki hii pamoja na wabunge wa Congress ya Marekani kusaka mbinu na njia za kutunga mkakati wa kukabiliana na msukosuko ulioyakumba mabenki hata kufilisika .Walikutana kwan za jana usiku na viongozi wa Congress lakini hawakuzungumzia moja kwa moja kuanzisha mfuko kuyatia jeki mabenki yanayoyumbayumba.

Mtaalamu wa mikakati ya raslimali Dariusz Kowalczyk amesema kwamba hatua hizi zinazochukuliwa sasa ni kali zaidi kuliko zuile za awali za kutia viraka hapa na pale na ndio maana zimeanza sasa kuleta tija kwa kufufua masoko ya fedha.Aliongeza lakini kusema kuwa ni vigumu kujua kwa muda gani hali hii ya kufufuka kwa masoko ya hisa na fedha itadumu,lakini anatumai hali sasa itakua bora kuliko ilivyokua.

Hisa barani Asia nazo zimepanda zaidi kutoka pale masoko ya fedha ya Marekani yalipoacha hapo kabla huku kipimo cha MSCI INDEX kinachobainisha hali ya masoko ya Asia mbali na Japan yalivyo,kubainisha muongezeko wa 5.7%.Hisa katika masoko ya Tokyo, zilipanda kwa kima cha 3.3%.

Kipimo cha Shanghai ,nchini China, kilipanda kwa hadi 9.5%-hii ni baada ya serikali ya China kujitia kati kwa hatua zake za mageuzi ili kuzuwia kuteremka kwa hadi 69% kutoka kiwango cha juu kabisa cha rekodi cha Oktoba mwaka jana.

Wakati fulani jana kabla hali haikuanza kupambazuka, hisa za Morgan Stanley zilishuka hadi kufikia 42% na zile za Goldman hadi 25% na kuchangia zaidi katika msukosuko wa siku kadhaa ulioteketeza mabilioni ya dala kwenye masoko ya fedha.

Lakini baada ya kutoka taarifa za hatua zinazochukuliwa na serikali ya Marekani na Uingereza,mashirika hayo ya fedha yalipata nafuu na yakifanya biashara nono zaidi.

Wawekezaji wakijifunza darasa kutoka kimbunga hiki kilichovuma kwenye masoko ya fedha, wameanza kujiuliza iwapo mfumo wa raslimali unaotumiwa na mabanki unafaa kuendelea kutumika baada ya kufilisika mapema wiki hii kwa Banki moja kubwa -Lehmann Brothers Holdings.Kumekuwapo pia uvumi kuwa Goldman,Banki kubwa kabisa na lenye nguvu mno -ambalo wakati mmoja likionekana haliguswi, linabidi sasa kutafuta mshirika.