1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatoa habari juu ya mtambo wake wa pili wa madini ya uranium

Abdu Said Mtullya25 Septemba 2009

Iran yatoa habari juu ya mtambo wake wa pili wa madini ya uranium!

https://p.dw.com/p/JpE7
Mtambo wa kurutubishia madini ya uranium nchini Iran.Picha: AP

Iran imetoa taarifa kwa Umoja wa Mataifa kwamba inajenga mtambo mwingine wa kurutubishia madini ya uranium yanayoweza kutumiwa kwa ajili ya kuundia silaha za nyuklia.

Lakini Iran imechelewa kutoa taarifa hiyo na nchi za magharibi zimekasirishwa.

Iran imetoa taarifa hiyo kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalodhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia IAEA.

Taarifa hiyo iliochelewa imewakasirisha viongozi wa nchi za magharibi na imeongeza wasi wasi wa viongozi hao juu ya nyendo za siri za Iran zinazoelekezwa katika shabaha ya kuunda silaha za nyuklia.

Iran ilitoa taarifa juu ya mtambo huo mwingine wa nyuklia katika barua kwa mkurugenzi mkuu wa shirika la IAEA bwana Mohammed Elbaradei iliyowasilishwa jumatatu iliyopita. Barua hiyo imewasilishwa wakati ambapo jopo la madola sita linajitayarisha kukutana na Iran tarehe mosi mwezi ujao.

Nchi za magharibi zimeishutumu Iran kwa kufanya udanganyifu.Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown ameilamu nchi hiyo kwa kuficha mipango yake ya kuunda silaha za nyuklia. Waziri Mkuu Brown ameeleza kuwa jumuiya ya kimataif sasa ipo tayari kuweka vikwazo madhubuti zaidi dhidi ya Iran.

Akizungumzia juu ya mtambo huo wa pili wa Iran rais Barack Obama wa Marekani amesema Iran pia ina haki ya kuwa na nishati ya nyuklia kwa shabaha za amani ili kukidhi mahitaji ya watu wake lakini mtambo huo wa pili hautangamani na shabaha za amani.Rais Obama amesema mtambo huo mpya unaaminika kuwa umejengwa ili kuwa na ujazo wa kuwa na mashine 300 za kurutubishia madini ya uraniamu.

Kwa mujibu wa wataalamu ikiwa mashine hizo zinawashwa kwa muda wote zinakuwa zinapata uwezo wa kuzalisha nyenzo za kutengenezea bomu moja la nyuklia kila mwaka.

Lakini Iran imekanusha madai kwamba ilificha habari ya juu ya mtambo huo mpya Afisa mmoja wa ngazi za juu ameliambia shirika la habari Reuters kwamba laiti mtambo huo ungelikuwa unaendeshwa kwa siri, basi Iran isingelitoa taarifa juu yake kwa shirika la IAEA.

Hadi sasa ni mtambo mmoja tu wa Iran wa Natanz unaojulikana na jumuiya ya kimataifa.

Mwandishi/ Mtullya Abdu/Reuters

Mhariri/.Abdul-Rahman