1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtandao nchini Sierra Leone waleta shida na mafanikio

Dirk Bathe / Maja Dreyer28 Juni 2007

Mnamo mwaka 1996, katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, shirika la kiserikali ya mawasiliano ya simu, iliadhimisha siku ya kwanza ya tovuti. Wakati huo, Sierra Leone ilikuwa moja kati ya nchi 11 barani Afrika ambazo ziliunganishwa na mtandao huo wa ulimwengu. Leo, miaka mitano baada ya kumalizika vita, Sierra Leone bado ni nchi maskini sana. Matumizi ya tovuti yameenea, lakini shida ni kubwa.

https://p.dw.com/p/CHkM

James Bognaby amekata tamaa. Akitumia tochi anajaribu kukarabati jenereta mbili wakati mmoja.

“Nini kimetokea? Kawaida tunazitumia jenereta hizo mbili wakati umeme unapokatika. Lakini sasa zote mbili zimeharibika na hatuwezi tena kuwahudumia watu kabla hatujakarabati mojawapo.”

Bw. Bognaby anaendesha mkahawa wa mtandao wa Internet, yaani Cyber Cafe katika mji mkubwa wa Bo. Huduma za umeme ni mbaya sana, mara nyingi umeme haupatikani kwa siku kadhaa.

Wakati huo huo, James Bognaby ni mmoja wa mameneja wa shirika la “Access to Afrika.com” lenye idadi kubwa ya mikahawa ya mtandao wa Internet katika eneo la Afrika Magharibi. Makao makuu ya shirika hilo yako nchini Marekani kwa sababu za usalama wa kisheria. Mikahawa iko pia nchini Nigeria na Kamerum. Lakini huko Sierra Leone ni vigumu zaidi kufanya biashara katika mikahawa ya mtandao. Bw. Bognaby anaeleza: “Kwangu mimi kama mfanyibiashara kukatikwa umeme ni athari kubwa. Naona wateja wanaokuja lakini sipati hela. Kwa hivyo, kwangu mimi sina raha hapa.”

Usiku kuchwa James Bognaby na wenzake wanazirekebisha jenereta. Asubuhi zinafanya kazi tena.

Mmoja ambaye anatumia tovuti sana ni Max Mohammed Kenne. Yeye mtaalamu wa maendeleo katika maeneo ya mashambani ambaye anafanya kazi katika Mashariki mwa nchi hiyo. Huko watu wengi wanajaribu kutafuta almasi, lakini ni wachache ambao wanapata pesa ya kutosha kuishi.

Max Mohammed Kenne anaendesha mradi wa shirika la Kijerumani la GTZ ambao unawafundisha vijana katika kazi ya ukulima. Kwa ajili hiyo, Max anategemea habari nyingi, ikiwa ni kuhusu elimu ya kilimo au bei za mbegu. Habari hizo anazipata kupitia mtandao: “Yote yanahusu kazi yangu. Ninawasiliana na wenzangu walioko nchi za nje. Wengine wanafanya na taasisi fulani barani Afrika na ninasoma tovuti zao kwenye Internet. Lakini tovuti pia inaniwezesha kuwasiliana na jamaa zangu walioko nje.”

Wale walio na laini ya mtandao nyumbani ni wachache tu. Hata wakiwa nayo, maunganisho yako polepole sana licha ya bei kuwa kubwa sana. Kwa mwezi, bei ni Dola 30 kwa saa mbili za kutumia Internet kila siku.

Mjerumani Manfred Rickert ambaye anafanya kazi Sierra Leone kama mwalimu, anayo kompyuta nyumbani, hata hivyo anaenda Cyber mara nyingi: “Ikiwa inabidi kutafuta habari kwa ajili ya semina au warsha, naenda Cyber ambapo Internet inakwenda haraka zaidi. Ni ghali, lakini hata hivyo naenda huko kwa sababu katika ofisi kazi hii ya utafiti haiwezekani. Inachukua muda mrefu mno mpaka ukarasa mmoja unaonekana.”

Bei kubwa na ubora mbaya wa maunganisho ndizo sababu, kwa nini watu kama Manfred Rickert hawaamini, mtandao utatumika na watu wengi katika nchi maskini kama Sierra Leone.