1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtazamo wa Ulaya kuhusu uchaguzi wa Ujerumani

Daniel Gakuba
22 Septemba 2017

Tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi nyingine zilizoleta wasiwasi barani Ulaya mwaka huu, hakuna hofu yoyote ya kitisho cha itikadi kali wala udukuzi wa Urusi kuhusiana na uchaguzi ujao nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2kWWY
Würfelspiel um Deutschland Symbolfoto Angela Merkel Martin Schulz
Ulaya inahitaji uongozi imara kwa Ujerumani, kwa sababu siasa za Ujerumani zinaiathiri Ulaya nzimaPicha: picture-alliance/U. Baumgarten

Ukweli kwamba kinyang'anyiro cha ukansela kinawakutanisha Angela Merkel, kinara wa maamuzi katika Umoja wa Ulaya, na Martin Schulz ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Ulaya, na kwa kuzingatia umuhimu wa Ujerumani kiuchumi na kisiasa ndani ya Umoja wa Ulaya, vingetoa hisia ya mchuano mkali, ambao ungefuatiliwa kwa karibu na kila mtu barani Ulaya, ambaye anafahamu kuwa mustakabali wake unafungamanishwa na Ujerumani.

Lakini hiyo sio hali halisi.

Mdahalo pekee wa televisheni uliowaleta pamoja Merkel na Schulz ulikosolewa kwa kukosa tofauti kimawazo, baadhi wakisema ulikuwa kama maongezi tu kati ya wagombea wenye mtazamo sawa, kiasi cha kuwafanya wapigakura washindwe kuamua yupi wa kumchagua.

Utafiti wa maoni ya wapiga kura unaonyesha kuwa Bi Merkel atashinda uchaguzi huu bila ya taabu, hali inayowanyima msisimko wanaofuatilia uchaguzi huo ndani na nje ya Ujerumani.

Lakini Sophia Besch kutoka kituo cha Mageuzi ya Ulaya, anasema yapo masuala muhimu ambayo yanapaswa kuangaziwa zaidi.

''Kiukweli hakuna mjadala barani Ulaya kuhusu uchaguzi huu wa Ujerumani. Yapo masuala kadhaa ambayo yanaihusu Ulaya katika sera ya nje ya Ujerumani mnamo miaka miwili hivi ijayo. Tumeshuhudia mahusiano kati ya Ujerumani na Uturuki yakiharibika haraka, na upo bado mzozo wa wakimbizi, na namna ya kuimarisha ulinzi wa Ulaya.'' Amesema Bi Besch.

Baadhi bado wanakasirishwa na sera ya Merkel kuhusu wakimbizi

Deutschland Aufnahmestelle für Flüchtlinge Zirndorf
Uamuzi wa Kansela Merkel kukaribisha mamia ya maelfu ya wakimbizi nchini Ujerumani ulimtikisa kisiasaPicha: picture-alliance/dpa/D. Karmann

Uamuzi wa Kansela Angela Merkel kuwaruhusu wakimbizi takribani milioni moja kuingia Ujerumani mwaka 2015, ndilo suala linalofuatiliwa sana barani Ulaya, na kuna wakosoaji ambao wangefurahi kama lingemuangusha katika uchaguzi ujao.

Katika mjadala ulioandaliwa na Televisheni baada ya mdahalo kati ya Bi Merkel na Bwana Schulz, Kosma Zlotowski ambaye ni mbunge wa Poland katika Bunge la Ulaya, alisema uamuzi huo wa Kansela Merkel ulikiuka misingi ya Umoja wa Ulaya.

Amesema, ''Mshikamano ni pale panapokuwepo mjadala. Lakini uamuzi wa kuwaingiza wakimbizi milioni moja na nusu nchini Ujerumani ulifanywa na Kansela Merkel binafsi. Yeye ni yeye, hakumuuliza mtu alipoamua.''

Kiongozi wa Ujerumani ni kiongozi wa Ulaya pia

Mbunge wa Slovenia katika Bunge la Ulaya Tania Fajon, anasema hali inamulika tatizo la nchi nyingine za Ulaya, kwamba Ujerumani inayo kauli nzito zaidi katika maamuzi ya Umoja wa Ulaya.

''Hali halisi ya leo ni kwamba kila uamuzi unaochukuliwa mjini Brussels unatanguliwa na kupiga simu mjini Berlin. Sitaki kuona Ujerumani ikiwa na uongozi dhaifu'', amesema Fajon na kuongeza, ''tunaongozwa na Ujerumani, ndio maana tunataka uongozi imara kwa Ujerumani, kwa sababu sio uongozi wa nchi hiyo pekee.''

Sophia Besch kutoka Kituo cha mageuzi ya Ulaya anasema Martin Schulz ameshindwa kutumia umaarufu alioupata alipokuwa spika wa Bunge la Ulaya kuimarisha kampeni ya ukansela nchini mwake, na sasa atashindwa na Bi Merkel. Besch anasema hali hiyo inaweza kumnufaisha Kansela Merkel, lakini hali ya kuwa na upinzani dhaifu haina tija kwa demokrasia ya Ujerumani.

 

Mwandishi: Teri Schulz

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman