1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mto Zambezi na kinyanganyiro cha maji

16 Machi 2009

Kutoka jumla ya kama mito 260 inayojulikana kimataifa,zaidi ya 60 ipo katika Bara la Afrika.Vile vile eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ni eneo lenye maziwa na mito mingi inayovuka mipaka.

https://p.dw.com/p/HCrG

Lakini kwa kudra ya kijiografia baadhi ya nchi zinapata maji mengi na hupakana na nchi zenye ukame.Nchi hizo kwa sehemu kubwa hutegemea maji yanayotoka upande wa pili wa mipaka yake - hali iliyosababisha matatizo kusini mwa Afrika.Miongoni mwa mito inayovuka mipaka ni Mto Zambezi,mto mkubwa wa nne barani Afrika ukiwa na urefu wa kilomita 3,000. Mto Zambezi unavuka mipaka ya nchi nane,ukipitia kwa sehemu kubwa nchini Zambia,ikifuatwa na Angola,Zimbabwe,Msumbiji,Malawi,Tanzania,Botswana na Namibia. Miongoni mwa nchi zilizorutubika kwa mto Zambezi ukipitia upande wa magharibi ni Angola na Zambia.Lakini unakopitia upande wa mashariki huko Msumbiji mto huo hauna maji mengi hivyo.Na hilo ni tatizo.Kwa mfano katika baadhi ya nchi kunakopita Mto Zambezi kuna wasiwasi kuwa Angola iliyoshinda kutumia raslimali yake ya maji wakati wa vita vya wenywe kwa wenyewe,sasa huenda ikaanzisha miradi mipya kama vile ujenzi wa mabwawa na kuzidisha matumizi yake ya maji.

Miradi kama hiyo itaathiri nchi za bondeni zinazotegemea maji kutoka Mto Zambezi kama vile Msumbiji na kuna hatari ya kuzuka kwa migogoro katika maeneo kama hayo.Isitoshe,Namibia inataka kupanua mfumo wa umwagiliaji maji kwa ajili ya mashamba yake ya miwa kwenye eneo la Caprivi;Botswana nayo inajenga bomba la kupeleka maji hadi mji mkuu Gabarone. Zimbabwe pia inataka kukidhi mahitaji ya jiji kubwa la Bulawayo.Miradi hiyo yote humaanisha kuwa Malawi ikiwa bondeni sehemu ya mwisho ya Mto Zambezi,ndio itakayopungukiwa maji.Lakini hata nchi isiyopakana na Mto Zambezi inataka kuutumia mto huo kama anavyoeleza Lars Wirkus wa kituo cha kimataifa cha BICC mjini Bonn.Anasema:

"Hata Afrika Kusini inataka kuutumia Mto Zambezi.Inataka kujenga bomba litakalosafirisha maji kutoka mto huo hadi Afrika Kusini likiwa na urefu wa kilomita 1,200 ili kuhakikisha kuwa katika siku zijazo,viwanda vyake wilayani Gauteng vitakuwa na maji ya kutosha."

Uwezekano wa migogoro kuripuka katika kanda hiyo ni mkubwa.Kwa hivyo ni muhimu kwa nchi ambako Mto Zambezi hupitia kushirikiana na kutumia maji ya mto huo kwa uangalifu.