1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtu aliyehusika na shambulio la bomu dhidi ya ndege ya PanAm huenda akaachiwa huru

Sekione Kitojo13 Agosti 2009

Mhusika katika shambulio la bomu dhidi ya ndege ya PanAm nchini Scotland huenda akaachiliwa huru kutokana na sababu za kiutu.

https://p.dw.com/p/J8sH
Abdel Basset Ali al-Megrahi, mmoja kati ya watuhumiwa wawili kutoka Libya wanaotuhumiwa kufanya shambulio la bomu dhidi ya ndege ya shirika la ndege la Pan Am katika anga ya Lockerbie, Scotland mwaka 1988.Picha: AP

Ripoti za televisheni nchini Uingereza zinasema kuwa mtu aliyehukumiwa kifungo cha maisha kwa kuhusika na shambulio la bomu dhidi ya ndege ya shirika la ndege la Marekani Pan Am katika eneo la Lokerbie nchini Scotland Abdelbasset Ali al-Megrahi anatarajiwa kuachiwa huru kutoka jela nchini Scotland kwa msingi wa huruma, lakini waziri anayehusika na uamuzi kuhusu hatma ya al-Megrahi amekana kuwa uamuzi kama huo umefanyika.

Ndugu wa watu 270 waliouwawa katika shambulio la bomu dhidi ya ndege ya shirika la ndege la Pan Am katika anga ya Lockerbie nchini Scotland, leo Alhamis walitoa majibu mchanganyiko kuhusiana na ripoti kuwa raia wa Libya aliyehukumiwa kuhusika na shambulio hilo anaweza kutolewa kutoka jela hivi karibuni.

Vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti jana Jumatano kuwa Abdel Basset al-Megrahi , ambaye anatumikia kifungo cha maisha katika jela ya Greenock karibu na mji wa Glasgow, ataachiliwa huru wiki ijayo. Anaugua saratani ya kibofu.

Uamuzi wa kumuacha huru al-Megrahi umo mikononi mwa waziri wa sheria wa Scotland Kenny MacAskill, ambaye wiki iliyopita alimtembelea raia huyo wa Libya jela mjini Glasgow na pia alikutana na familia za wahanga.

Lakini serikali ya Scotland imekana ripoti hizo kuwa uamuzi umefanyika kumwacha huru al-Megrahi. Msemaji wa mkuu wa serikali ya jimbo huko Scotland Alex Salmond, ameieleza ripoti hiyo kuwa ni uvumi mtupu.

Hakuna uamuzi uliofanyika , ama ombi la kuachiwa kwa raia huyo wa Libya kwa misingi ya huruma ama kuna makubaliano chini ya msingi wa uhamisho wa wafungwa kwa hiyo huo ni uvumi mtupu, amesema.

Jim Swire ambaye ni daktari, ambaye amempoteza mwanae wa kike katika shambulio hilo la bomu, amesema kuwa anaukaribisha uamuzi wa kuachiwa na mapema kwa al-Megrahi. Haamini kuwa hukumu aliyopewa ilikuwa sahihi. Mimi ni mtu ambaye si amini kuwa anahatia. Ni bora arejea katika familia yake. Itakuwa ni ukatili mkubwa kumuacha afie jela, Swire amekiambia kituo cha televisheni cha BBC.

Lakini nguvu wa wahanga waliouwawa katika shambulio hilo kutoka Marekani walitoa maelezo tofauti.

Susan Cohen, ambaye mwanae wa kike alikuwa mhanga wa shambulio hilo, amesema kuwa ushauri kuwa al-Megrahi anapaswa kuachiliwa huru kwa misingi ya huruma ni wa kuchukiza.

Cohen amesema serikali ya Uingereza itakuwa inafanya usaliti kwa wahanga wa Lockerbie iwapo itaamua kumuacha huru al-Megrahi, ambaye alihukumiwa katika kesi iliyofanyika nchini Uholanzi mwaka 2001 chini ya sheria za Scotland. Majaji wameamua kuwa atabakia jela kwa kipindi cha wastani wa miaka 27.

Al-Megrahi amekuwa mara zote akilalamika kuwa hana hatia na alianzisha hatua mpya ya kukata rufaa dhidi ya hukumu yake mapema mwaka huu. Mchunguzi wa umoja wa mataifa na tume ya kupitia upya kesi za uhalifu nchini Scotland wamesema kuwa kuna wasi wasi mkubwa kuwa raia huyo wa Libya anaweza kuwa mhanga wa kutotendewa haki kisheria.

Mwandishi Sekione Kitojo/DPAE

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman