1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtu aliyeuwa Munich ana uraibu wa mihadarati

Admin.WagnerD10 Mei 2016

Imefahamika kuwa yule mshambuliaji aliyemuua mtu mmoja kwa kisu na kuwajeruhi wengine watatu kusini mwa Ujerumani mapema leo ana matatizo ya kiakili na pia mtumiaji wa madawa ya kulevya.

https://p.dw.com/p/1IlCd
Deutschland Messerattacke am Grafinger Bahnhof
Aliyeshambulia kwa kisu ni mraibu wa mihadaratiPicha: Reuters/M. Rehle

Polisi wamemkamata mtu huyo mwenye umri wa miaka 27 baada ya shambulio hilo katika kituo cha treni cha Grafing, mashariki mwa mji wa Munich.

Mmoja wa wahanga, mwenye umri wa miaka 56, alifariki baadaye hospitalini kutokana na majeraha aliyoyapa. Maafisa hapo kabla walisema kimakosa kwamba umri wake ni miaka 50.

Deutschland Messerattacke am Grafinger Bahnhof
Kituo cha Grafing kulikotokea shambulio la kisuPicha: picture-alliance/AA/L. Barth

Wengine waliojeruhiwa walikuwa wanaume wenye umri wa miaka 43, 55 na 58. Mmoja kati ya wahanga alijeruhiwa vibaya , wengine wawili wamepata majeraha madogo madogo.

Polisi na waendesha mashitaka awali walisema shambulio hilo linaonekana kuwa na "ushawishi wa kisiasa" na lengo la itikadi kali ya Kiislamu baada ya watu walioshuhudia kuripoti kwamba walisikia akipiga kelele "Allahu Akbar" Mungu mkubwa.

Ushahidi

Hata hivyo, saa chache baadaye, wizara ya mambo ya ndani katika jimbo la Bavaria limesema kwamba "hadi sasa hatuna ushahidi wa ushawishi wa itikadi za Kiislamu, lakini uchunguzi unaendelea."

Deutschland Messerattacke am Grafinger Bahnhof
Maua yamewekwa katika tukio la shambulioPicha: picture-alliance/AA/L. Barth

"Tumegundua kwamba mtu huyo ana matatizo ya akili na matumizi ya madawa ya kulevywa," msemaji wa wizara Oliver Platzer ameliambia shirika la habari la AFP.

Waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya shirikisho Thomas de Maiziere amesema kwamba.

Lilikuwa ni shambulio la uoga na linalochukiza ambalo limeuwa mtu mmoja. Fikira zangu ziko pamoja na ndugu,wa waliojeruhiwa, nawatakia kupona kwa haraka. Sababu za shambulio hili bado hazijafahamika,maafisa wa ofisi ya mwendesha mashitaka ya Bavaria imetoa taarifa na,kutoka Berlin sitaki kuchochea na kutathmini uvumi juu ya lengo la shambulizi hilo."

Mshambuliaji raia wa Ujerumani

Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria Joachim Herrmann amesema mshambuliaji , ambaye ametambulika kwa jina la Paul H. ni raia wa Ujerumani, kama maafisa wanavyosema anatokea katika jimbo la kati la Hesse na hana asili ya wahamiaji.

"Kutokana na kiasi gani kuna vitu vinavyohusika katika asili yake, ama iwapo hili ni suala zaidi la uraibu wa madawa ya kulevywa na matatizo ya akili, bado kuna haja ya uchunguzi," Herrmann amesema katika televisheni ya BR24.

Deutschland Messerattacke am Grafinger Bahnhof
Kituo kimefungwa baada ya tukioPicha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Hapo mapema Ken Heidenreich , msemaji wa ofisi ya mwendesha mashitaka , alisema kwamba "mshambuliaji alitoa matamshi katika eneo la tukio ambayo yanaashiria lengo la kisiasa, hususan lengo la itikadi kali ya Kiislamu.. Bado tunatafakari ni matamshi gani aliyatoa.

Katika shambulio hilo lililotokea asubuhi , mshambuliaji alimchoma kisu mtu mmoja ndani ya treni, mwingine kituoni, na kisha aliondoka katika kituo hicho cha treni na kuwakata visu watu wengine wawili waliokuwa wakiendesha baisikeli , amesema msemaji wa polisi ya Bavaria Karl-Heinz Segerer.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Mohammed Khelef