1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa muuwaji afikishwa mahakamani

25 Julai 2011

Anders Behring Breivik amefikishwa mahakamani mjini Oslo.Mashambulio ya Norway yamewazinduwa pia wanasiasa wa nchi jirani juu ya kitisho cha mashambulio ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.

https://p.dw.com/p/1235o
Mtuhumiwa Behring Breivik (kushoto)apelekwa mahakamaniPicha: dapd

Anders Behring Breivik aliingia na kutoka kupitia mlango wa nyuma wa mahakama akiwa ndani ya gari lililoshamiri silaha.

Hapajapita muda mrefu kikao kikamalizika-kilidumu dakika 40 tu.Amesema hayo afisa mmoja wa mahakama katika mji mkuu wa Norway-Oslo.

Jaji Kim Heger aliitika mwito wa mwendesha mashtaka kutaka kesi hiyo isikilizwe kwa siri pamoja pia na mtuhumiwa huyo kuendelea kushikiliwa kwa wiki nane huku uchunguzi ukiendelea kufanywa.Muda huo unaweza kurefushwa ikihitajika.

"Mtuhumiwa ametoa ripoti zinazohitaji uchunguzi ziada,ikiwa ni pamoja na ile hoja kwamba kuna makundi mawili zaidi anayoshirikiana nayo"! amesema jaji Kim Heger mbele ya waandishi habari.

Jaji Kim Heger amesema Breivik atafungwa peke yake,hatotembelewa na watu isipokuwa wakili wake tu.

Anders Behring Breivik amekiri ameuwa lakini anasema hajafanya uhalifu wowote.Anahoji mashambulio yake yamelenga kuikoa Ulaya dhidi ya dini ya kiislam.

Norwegen nach den Anschlägen in Oslo und Utøya Schweigeminute
Kutoka kushoto:Mfalme Harald, malikia Sonja, mwanamfalme Prince Haakon na waziri mkuu Jens StoltenbergPicha: dapd

Kabla ya hapo wanorway walikaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa mashambulio ya kigaidi ya ijumaa iliyopita huko Oslo na katika kisiwa cha Utoya.Pirika pirika zote za maisha ikiwa ni pamoja na safari za reli zilisita saa sita ilipogonga.

Umati wa watu walimshangiria mfalme Harald wa tano,malkia na waziri mkuu Jens Stoltenberg walipowasili katika chuo kikuu cha Oslo kutia saini daftari la maombolezi kwaajili ya wahanga na familia zao.

Rambi rambi zimetolewa pia katika nchi jirani za Sweeden,Finland, Danemark na kwengineko barani Ulaya.

Wolfgang Bosbach
Wolfgang Bosbach wa kutoka chama cha CDUPicha: picture-alliance/ dpa

Mwenyekiti wa kamati ya mambo ya ndani ya bunge la shirikisho Bundestag Wolfang Bosbach haondowi uwezekano wa kutokea shambulio kama lile la Norway nchini Ujerumani.

Nnaamini kila kitu kitafanywa hivi sasa nchini Norway ili kuona kama mtuhumiwa huyo alikuwa akiwasiliana na makundi mengine ya watu.Kwa mtazamo wa Ujerumani ni muhimu kujua kama alikuwa na mawasiliano kwa mfano na makundi ya siasa kali ya mrengo wa kulia nchini Ujerumani.Data za mawasiliano ya simu zinaweza kusaidia upande huo.

"Ni shambulio linalokwenda kinyume na maadili ya nchi zetu.Ni shambulio dhidi yetu sote" amesema kwa upande wake waziri mkuu wa Danemark Lars Loekke Rasmussen.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/afp

Mhariri Yusuf Saumu