1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa wa mauaji ya Charleston kufunguliwa mashtaka

22 Juni 2015

Kijana mmoja wa Kizungu anayetuhumiwa kwa kuwaua kwa kuwapiga risasi watu tisa katika kanisa moja la kihistoria la Wamarekani weusi, katika jimbo la South Carolina ametiwa nguvuni.

https://p.dw.com/p/1Fjcb
USA Schießerei in einer Kirche in South Carolina Reaktionen
Picha: Reuters/B. Snyder

Rais wa Marekani Barack Obama ametoa wito kwa viongozi kutafakari kuhusu sheria za udhibiti wa bunduki.

Mkasa huo ulisababisha msako mkali wa saa 14 ambao uliwezesha kukamatwa mshukiwa wa mauaji hayo Dylann Roof, mwenye umri wa miaka 21 katika kituo kimoja cha trafiki cha mji mdogo wa jimbo la North Carolina, karibu kilomita 350 kaskazini mwa Charleston, ambako tukio hilo lilitokea.

Roof, ambaye mjombake amesema alizawadiwa bastola wakati alitimiza umri wa miaka 21 mwezi Aprili na ambaye maelezo yake kwenye mtandao wa kijamii yanaonyesha ana itikadi za chuki dhidi ya weusi, alirejeshwa katika jimbo la South Carolina saa chache baada ya kukamatwa. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kwa ajili ya kusikizwa kesi yake, lakini atatumia njia ya video kutoka eneo la Charleston ambako amewekwa kizuizini.

Polisi imesema ufyatuaji huo wa risasi ulianza karibu saa moja baada ya Roof kujiunga na kikundi kidogo cha waumini wa kanisa hilo waliokuwa kwenye mafunzo ya bibilia ndani ya kanisa hilo, aliyekaribishwa kama mshiriki pekee mzungu na kisha akawafyatulia risasi wahanga hao walipokuwa wameketi pamoja.

USA Schießerei in einer Kirche in South Carolina Reaktionen
Waumini wakifanya ibada ya kuwakumbuka wahanga tisa waliopoteza maisha na kujeruhiwaPicha: Reuters/G. Beahm

Wachungaji wanne, akiwemo Seneta wa chama cha Democratic Clementa Pinckney, mwenye umri wa miaka 41, ni miongoni mwa wanawake sita na wanaume watatu waliouawa kwa kupigwa risasi ndani ya kanisa hilo la African Methodist Episcopal.

Obama akasirishwa na mauaji

Rais Barack Obama ameelezea hasira yake kuhusiana na tukio hilo akisema kuwa Wamarekani wanapaswa kufahamu ukweli kuwa matukio ya mara ya kwa mara ya mauaji ya aina hiyo hayatokei katika mataifa mengine yaliyoendelea.

"Nimetoa kauli kama hizi mara nyingi sana. Jamii kama hii zimekumbwa na mikasa kama hii mara nyingi. Acha tuwe wazi, ufike wakati ambapo kama nchi tutalazimika kufahamu ukweli kwamba mauaji kama haya ya watu wengi hayafanyiki katika nchi nyingine zilizoendelea. Hayafanyiki katika maeneo mengine kwa kiwango hiki, na tuna nguvu za kuchukua hatua"

Marekani imetikiswa na msururu wa matukio ya ufyatuaji rsasi katika miaka ya karibuni, ikiwa ni pamoja na mauaji ya mwaka wa 2012 katika Shule ya Sandy Hook, ambako mtu aliyekuwa na bunduki aliwauwa watoto 20 na watu sita wazima. Lakini juhudi za Wademocrat za kuimarisha sheria za udhibiti wa bunduki nchini humo zikashindwa baada ya tukio hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Josephat Charo