1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa gaidi akamatwa

Oumilkheir Hamidou
10 Oktoba 2016

Polisi nchini Ujerumani wamemkamata mkimbizi wa Syria aliyekuwa akisakwa tangu siku mbili zilizopita kwa tuhuma za kuandaa shambulio la kigaidi.

https://p.dw.com/p/2R4cN
Eneo alikokamatwa gaidi mtuhumiwa,katika mji wa Leipzig
Eneo alikokamatwa gaidi mtuhumiwa,katika mji wa LeipzigPicha: picture-alliance/dpa/H. Schmidt

.

"Tumefanikiwa,na tumeshusha pumzi,mtuhumiwa wa kigaidi Jaber Albakr amekamatwa jana usiku mjini Leipzig"- katika jimbo la Saxony,polisi imesema kupitia mtandao wa kijamii Twitter

 Kijana huyo mwenye umri wa miaka 22  alikimbilia katika nyumba ya msyria mwenzake aliyemkuta katika kituo cha safari za treni cha Leipzig na kumuomba amkaribishe kwake-hayo lakini ni kwa mujibu wa mtandao wa jarida la der Spiegel.

Raia huyo wa Syria alikubali kumkaribisha,lakini pia aliwapigia simu polisi baada ya kusikia kwamba kijana huyo anasakwa na polisi. Mji wa Leipzig hauko mbali na Chemnitz ambako Jaber Albakr alikuwa akiishi kama mkimbizi tangu zaidi ya mwaka sasa na ambako baruti ziligunduliwa ndani ya nyumba yake jumamposi iliyopita.

Vikosi maalum vya polisi vimemkuta mtoro huyo amefungwa miguu na mikono akiwa ndani ya nyumba alimokaribishwa.

Gaidi mtuhumiwa Jaber Albakr
Gaidi mtuhumiwa Jaber AlbakrPicha: picture-alliance/dpa/Polizei Sachsen

Majirani wanasimulia:"Tulikuwa na wasi wasi kidogo. Lakini ni vizuri  kusikia kwamba mtuhumiwa kakamatwa baada ya raia mwenzake kuijulisha polisi. Ni kitendo cha kishujaa. Heko. Anastahiki hishma zote kwa aliyofanya."

Leo mchana mtuhumiwa huyo atapelekwa Karlsruhe,makao makuu ya korti kuu ya Ujerumani -korti yenye jukumu la kushughulikia masuala ya ugaidi. Baadae utaitishwa mkutano na waandishi habari. Kwa mujibu wa duru za korti kuu ya shirikisho "kila kitu kinadhihirisha kwamba mtuhumiwa huyo alidhamiria kufanya shambulio la kigaidi."Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ujerumani,alilenga kuushambulia uwanja wa ndege au kituo cha usafiri.

Baadhi ya vyombo vya habari vinasema kijana huyo alikuwa na mshikamano na wanamgambo wa dola la kiislam IS waliomfundisha jinsi ya kutengeneza na kutumia miripuko.

Kukamatwa kwake,tukio lililojiri usiku wa jana kuamkia leo kunamaliza msako wa siku mbili wa vikosi vya usalama.

Mtaa alikokamatwa Jaber Albakr
Mtaa alikokamatwa Jaber AlbakrPicha: DW/N. Conrad

Kadhia hii imeanza ijumaa iliyopita baada ya idara ya upelelezi wa ndani iliyokuwa ikimchunguza Jaber Albakr kuwashauri polisi wa mji wa Chemnitz,mji ulioko umbali wa kilomita 260 kusini mwa mji mkuu Berlin,kumkamata kwa dhana za kuandaa shambulio la akigaidi.Vikosi vya usalama viliingilia kati mapema jumamosi iliyopita,lakini mtuhumiwa alifanikiwa kutoroka..Bbadala yake lakini wamegundua shehena kubwa ya miripuko.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef