1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa wa ujasusi aungama Marekani

Thelma Mwadzaya2 Julai 2010

Sakata la ujasusi kati ya Marekani na Urusi limechukua mwelekeo mpya baada ya mshukiwa mmoja kuungama pindi alipokamatwa.

https://p.dw.com/p/O8vX
Makazi ya Vicky Pelaez na "Juan Lazaro" walikokamatwa mjini New York.Picha: AP

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka wa Marekani, mtuhumiwa huyo alikiri kuwa anaiamini zaidi  serikali ya Urusi  kuliko mwanawe wa kiume. Hata hivyo, Rais Medvedev wa Urusi bado hajatoa kauli yoyote kuhusiana na kisa  hicho, ijapokuwa Waziri Mkuu, Vladmir Putin, aliyekuwa afisa wa ujasusi wa  zamani  katika  Idara ya KGB, amevikosoa vyombo vya sheria vya  Marekani. Kisa  hicho kinahofiwa kuwa huenda kikauathiri uhusiano wa kidiplomasia kati ya Urusi na Marekani.

Jina  la kughushi

Mtuhumiwa  huyo aliyetumia  jina lisilokuwa  la kweli la Juan  Lazaro, alieleza wazi kuwa mkewe, Vicky Palaez, ambaye  ni mwandishi aliyezaliwa nchini Peru, alifanya safari kadhaa kuelekea  Amerika ya Kusini kwa minajili ya kuwafichulia siri za kijasusi maafisa wa Urusi. Wawili hao ni sehemu ya watuhumiwa 11 waliohusika kwa njia moja au nyingine katika sakata  la  kuzifichua  siri za kijasusi  kati ya Marekani  na Urusi. Jambo  hilo  linahofiwa kuwa litaziathiri juhudi za kuuimarisha uhusiano  kati  ya mataifa hayo mawili.     

Tisa  kati yao wanaisubiri hatima yao  baada  ya kuyawasilisha maombi  ya kuachiwa kwa dhamana katika mahakama tatu tofauti. Wengine  watano, wanaousibiri  uamuzi  wa kisheria katika miji ya Boston na Virginia, wamelazimika kurejea tena mahakamani baada ya  kesi yao kuahirishwa ili kuipa nafasi ya kuutathmini ushahidi zaidi. 

USA Russland FBI har russisches Agentennetz ausgehoben
Picha ya Anna Chapman, (shoto), Vicky Pelaez, (wa pili ), "Richard Murphy",(kati) na "Cynthia Murphy", (pili kulia) na "Juan Lazaro" wakiwa mahakamani Manhattan,Newyork.Picha: AP

Barua  ya Lazaro

Mkuu  wa sheria wa mahakama ya jimbo  la kusini  la New  York, Preet Bharara, aliielezea  barua  ya Lazaro ya kuungama aliyoandikiwa Jaji  Ronald Ellis. Kulingana na  barua  hiyo, Lazaro alimuomba mwanasheria  huyo kutofanya kosa  kama lile lililotokea Cyprus  ambako mtuhumiwa  mmoja  muhimu  aliachiwa kwa dhamana na  baada ya hapo alitoweka. 

Katika taarifa  yake ya kina aliyoielezea  baada ya kuthibitisha  kuwa anazikanusha haki zake  kama mhalifu, kwa kufuata misingi ya katiba-maarufu onyo la Miranda- Lazaro alikiri kuwa hakuwa  raia  wa Uruaguay na kwamba Juan  Lazaro si jina lake la kweli. Hata hivyo, kamwe hakujitambulisha kikamilifu. Alifafanua kuwa ijapokuwa anampenda sana mwanawe wa kiume, kamwe hatoukiuka  wajibu wake  kwa idara ya  ujasusi ya Urusi, SVR, iliyozinduliwa baada ya ile ya  KGB ya wakati  wa utawala wa Kisovieti  kuvunjwa.

Kwa  upande wake, Jaji  Ellis alisema  kuwa atautangaza uamuzi wake baadaye, ila mkewe Lazaro,Vicky Pelaez,ataachiwa  kwa dhamana  ya  kiasi cha dola laki  mbili na nusu, na atazuiliwa nyumbani. Hiyo ni  kwa sababu Vicky Pelaez si jasusi na ana  jina la kweli  na anafahimika  kuwa ni raia  wa Marekani  aliye na haki  ya kuishi katika  nchi yoyote ile.

Maombi ya kuachiwa kwa dhamana

Yote  hayo yakiendelea, Jaji  Ellis  alilitupilia  mbali ombi la kuachiwa kwa dhamana watu wengine wawili, Richard na  Cynthia  Murphy, wanaotuhumiwa kutafuta mawasiliano  na maafisa wa  ngazi za juu tangu  miaka ya tisaini walipojifanya kuwa wakaazi  wa New Jersey.

Barua hiyohiyo aliyoandikiwa  Bharara ilieleza  pia kuwa shirika la ujasusi la Marekani, FBI, ilifanikiwa kufichua maandishi  ya  siri ambayo mpaka sasa  hayajatangaziwa  umma. Maafisa hao kadhalika walizipata barua 8  ambazo hazikuwa na maelezo zilikuwamo kiasi cha dola alfu kumi kumi za noti  za  dola mia.    

KGB Gebäude in Minsk
Majengo ya KGB,yaliyoko MinskPicha: Bymedia

Kwa  upande  mwengine, ombi la mtuhumiwa wa kumi, Anna Chapman, la kuachiwa  kwa dhamana lilitupiliwa mbali. Kwa mujibu wa taarifa  ya mume wake wa zamani Alex  Chapman,iliyochapishwa hii leo. kwenye  gazeti la Uingereza la Daily  Telegraph, wawili hao walikutana mwaka 2001 katika  hafla   moja mjini London.Kabla ya kuolewa aliitwa Anna Kushchenko.

Mume wake huyo  wa  zamani, Alex Chapman,alisema kuwa hakushangazwa na madai hayo ya kuhusika  na kashfa hiyo  ya kijasusi kwani Anna alishamdokezea kuwa babake  alikuwa  na nafasi ya  ngazi za  juu katika shirika la ujasusi la zamani  la Urusi, KGB. Alidai kwamba  alikuwa jasusi  wakati wa utawala wa  Kisovieti nchini Urusi. Alex Chapman alieleza kuwa baada ya  ndoa yao kusambaratika mwaka 2005,alihofia kuwa Anna  alikuwa anaandaliwa  kuwa jasusi. Kwa sasa Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza  inayachunguza madai hayo.

Mafichoni Cyprus

Mtuhumiwa wa 11 Christopher Metsos  alikamatwa Cyprus ila akatoweka baada ya kuachiwa kwa dhamana ya kiasi cha zaidi ya dola alfu 30 vilevile kuikabidhi mahakama hati  yake ya kusafiri.Inahofiwa kuwa  Metsos huenda akaelekea kwenye eneo  la kaskazini la kisiwa hicho kilicho karibu na bahari ya Mediterana,ambako   hakuna sheria zozote za kimataifa  za kuwarejesha kwao watuhumiwa.Ifahamike kuwa eneo  hilo linatumiwa sana kama maficho.

Katika kundi hilo ,watuhumiwa 9 huenda  wakahukumiwa   kifungo chahadi miaka 25 jela kwa mashtaka ya  ulanguzi wa  fedha  pamoja na  miaka  mitano  ya ziada kwa kukubali  kushirikiana  na serikali ya kigeni.Chapman na  mmoja  mwengine huenda wakakabiliwa  na mashtaka mepesi zaidi.Ifahamike kuwa hakuna yeyote kati yao anayekabiliwa na mashtaka  makali ya ujasusi.  

Mwandishi:Thelma Mwadzaya –AFPE

Mhariri: Miraji Othman