1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muasi wa zamani nchini Kongo afikishwa mahakamani Uholanzi

11 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D5eZ

Kiongozi wa zamani wa waasi anayeshtakiwa kwa mauaji ya wakongo 200 mnamo mwaka wa 2003, atafikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kwa mara ya kwanza hii leo mjini The Hague nchini Uholanzi.

Waongozaji mashitaka katika mahakama hiyo wanasema Mathieu Ngudjolo Chui, kiongozi wa kundi la waasi la FNI, aliviamuru vikosi vyake vikiangamize kijiji cha Bogoro, kaskazini mashariki mwa mkoa wa Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ngudjolo ataulizwa na mahakama ya mjini The Hague ikiwa anafahamu mashitaka yanayomkabili na atajulishwa haki alizonazo katika mahakama hiyo.

Mahakama hiyo inatarajiwa baadaye kuweka tarehe ya kusikilizwa kwa mashitaka hayo ambapo majaji wataamua mashtaka gani yatakayofunguliwa rasmi dhidi yake.