1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mubarak aapisha baraza 'jipya'

31 Januari 2011

Rais Hosni Mubarak ameliunda tena baraza lake la mawaziri, baada ya kulivunja Ijumaa iliyopita, ikiwa ni jitihada zake za kuitikia mwito wa waandamanaji, ambao wanamtaka yeye mwenyewe aondoke madarakani.

https://p.dw.com/p/107zF
Rais Hosni Mubarak akiwaapisha mawaziri 'wapya'
Rais Hosni Mubarak akiwaapisha mawaziri 'wapya'Picha: dapd

Leo Rais Hosni Mubarak ameliapisha baraza lake 'jipya' la mawaziri linaloongozwa na Waziri Mkuu Ahmed Shafiq, lakini ameshindwa kurudisha sura mpya, zaidi ya ile ya Mahmoud Wagby, anayechukua wizara ya ndani kutoka kwa Habib Al-Ahdy. Mawaziri wengine muhimu katika utawala wake, kama vile Mohammed Tantawi wa Ulinzi na Ahmed Aboul Gheith wa Mambo ya Nje, wamebakia kwenye nafasi zao, kama zilivyo kwa wizara za Mafuta na Ajira.

Vyanzo vilivyo karibuni na serikali, vimeliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kuwa maafisa wengi wa serikali wamekataa kujiunga na serikali hii, na huenda ikawa sababu ya Mubarak kurudi na sura kongwe kwenye baraza jipya.

Umoja wa Ulaya waonya

Catherine Ashton
Catherine AshtonPicha: AP

Wakati huo huo, jamii ya kimataifa imeendelea kumshinikiza Rais Mubarak ajiepushe na matumizi ya nguvu katika kukabiliana na waandamanaji, na achukuwe hatua za kurudisha demokrasia haraka.

Umoja wa Ulaya, kupitia Mkuu wake wa Sera za Nje, Catherine Ashton, umemtolea wito rais huyo, azuie damu zaidi isimwagike.

"Ninasikitishwa sana na upoteaji wa maisha ya watu, na idadi kubwa ya majeruhi. Ni muhimu kwa kila mmoja, hasa polisi, kujizuia na mashambulizi zaidi dhidi ya raia, ili kuepuka maafa zaidi." Amesema Bi Ashton.

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ameonya kuwa, kosa lolote litakalofanywa na uongozi wa Misri hivi sasa, litakuwa na athari ya moja kwa moja, kwa eneo la Mashariki ya Kati, Ulaya na dunia kwa ujumla.

Utalii na uwekezaji waathirika

Watalii waikimbia Misri
Watalii waikimbia MisriPicha: picture-alliance/dpa

Katika miji mikubwa kadhaa barani Ulaya hivi sasa, makampuni ya ndege na utalii yamelazimika ama kufuta safari zao au kufupisha likizo za wateja wao walioko Misri, kutokana na maandamano yanayoendelea huko kwa wiki nzima sasa.

Makampuni ya TUI na International Consolidated Airlines Group, tayari yamepoteza karibuni asilimia tatu za mauzo yake, huku ile ya Thomas Cook ikianguka kwa asilimia 2.2.

Katika uwanja wa ndege mjini Cairo mchana wa leo, mamia ya wageni, wakiwamo watalii na wawekezaji, wameonekana wakisubiri ndege za kuwarudisha makwao.

"Tunaondoka na familia yote leo hii, isipokuwa mume wangu tu anabakia kidogo kumalizia kushughulikia mambo yaliyobakia kwenye kampuni yetu, lakini naye ataondoka baadaye." Mwekezaji mmoja wa Kijerumani ameiambia DPA.

Hofu ya kuenea kwa machafuko katika eneo lote la Mashariki ya Kati na Kaskazini ya Afrika, ambako robo tatu ya mafuta duniani huzalishwa, imelikumba pia soko la mafuta duniani, ambako tayari pipa moja ya mafuta yasiyosafishwa, imeshafika dola 100 za Kimarekani.

Makampuni ya meli yao yasitisha huduma

Huko mjini Copenhagen, nchini Denmark, kampuni kubwa ya usafirishaji inayojishughulisha pia na biashara ya mafuta, A.P. Moeller-Maersk, imetangaza kusitisha shughuli zake nchini Misri, ingawa meli zake zitaendelea kupitia mfereji wa Suez, kwa sasa.

Msemaji wa kampuni hiyo, Michael Christian, ameliambia Shirika la Habari la AFP, kwamba wataitathmini hali hapo kesho, kuona ikiwa wafungue ofisi zao au la. Usitishaji huu wa kazi unawaathiri zaidi ya wafanyakazi 7,000 nchini Misri pekee.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdu-Rahman