1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mubarak Mahututi

20 Juni 2012

Wakati aliyekuwa rais wa Misri, Hosni Mubarak akiwa yu mahututi katika mojawapo ya hospitali ya kijeshi nchini humo.

https://p.dw.com/p/15IHi
Hosni Mubarak
Hosni MubarakPicha: picture-alliance/dpa

Bado taifa hilo lipo kwenye hali ya mashaka, ambapo tangu jana maelfu ya waandamanaji wamekusanyika katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo dhidi ya utawala wa kijeshi.

Watu walikusanyika tangu jana katika uwanja huo kuupinga vikali utawala wa kijeshi kwa kile kinachoonekana kusudio lake la kubaki madarakani, hata baada ya uchaguzi wa rais.

Mohammed Mursi, mgombea Urais kutoka chama cha udugu wa kiislamu.
Mohammed Mursi, mgombea Urais kutoka chama cha udugu wa kiislamu.Picha: picture-alliance/dpa

Tangazo la Baraza la Kijeshi

Tangazo la Jumapili la Baraza la Kijeshi ambalo lilisema wanajeshi wanajitwalia madaraka baada ya bunge kufutwa na mahakama ya kikatiba, ndio msingi wa maandamano hayo.

Chama cha Udugu wa Kiislamu, ambacho kilikuwa kinashikilia nusu ya viti kwenye bunge hilo, kimejiunga na waandamanaji hao.

´"Tunatamka bayana kuwa tunapinga kifungu cha ziada cha katiba na tunalitaka Baraza Kuu la Kijeshi kukabidhi madaraka mara moja kwa rais aliyechaguliwa." Aiman Sadek msemaji wa chama hicho alisema.

Matokeo yasiyo rasmi ya uchaguzi wa duru ya pili yanasharia kuwa Mohammed Mursi wa Udugu wa Kiislamu huenda akatangazwa mshindi, wakati matokeo rasmi yatakapotolewa hapo kesho.

Afya ya Mubarak

Wakati hali katika medani ya siasa ikiwa hivyo, hali ya afya ya aliyewahi kuwa rais wa taifa hilo, Hosni Mubarak, imezorota baada ya kuhamishiwa kutoka gerezani na kupelekwa kwenye hospitali ya kijeshi.

Uvumi umeenea kuwa kiongozi huyo wa zamani ambaye sasa anatumikia kifungo cha maisha, amekwishafariki dunia.

Hata hivyo, wakili wake, Farid al Deed, amesema licha ya afya Mubarak kuwa mbaya mno baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi kutokana na hali mbaya ya gerezani, bado angali hai. Mkewe, Suzanne Mubarak, ameripotiwa kwenda kwenye hospitali hiyo ya kijeshi kuangalia hali ya mumewe.

Mubarak akiwa na rais Obama, enzi akiwa rais wa Misri.
Mubarak akiwa na rais Obama, enzi akiwa rais wa Misri.Picha: Reuters

Mubarak alipelekwa gerezani kuanza kifungo chake cha maisha hapo Juni 2, baada ya mahakama kumtia hatiani kwa tuhuma kadhaa, zikiwemo za kuhusika na mauaji ya waandamanaji katika maandamano yaliyomuondoa madarakani. Yeye na aliyekuwa waziri wake wa mambo ya ndani walitiwa hatiani.

Matukio ya kumuua

Afya ya Mubarak aliyewahi kukoswakoswa kuuwawa mara10 akiwa madarakani, ilianza kuwa ya mashaka kutokana na ugonjwa wa moyo. Aliingia madarakani Oktoba 6, mwaka1981 mara baada ya kuuwawa kwa Rais wa Pili wa Misri, Anwar Sadat, aliyepigwa risasi na wanamgambo wa Kiislamu wenye misimamo mikali.

Miongoni mwa matukio aliyoponea kuwawa ni lile la mwaka 1993 nchini mwake na mwaka 1995 alipofurumishiwa risasi akiwa katika gari huko Addis Ababa, Ethiopia.

Mwandishi: Adeladius Makwega/DPAE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef