1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe asema hang'oki madarakani labda mungu apende

21 Juni 2008

-

https://p.dw.com/p/ENok

HARARE

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amewaambia wafuasi wake mjini Bulawayo kwamba hataondoka madarakani ila kwa amri ya mungu na kwamba chama cha MDC hakiwezi kuruhusiwa kwamwe kuitawala nchi hiyo.Chama hicho cha upinzani kwa upande wake kinajiandaa jumatatu kutangaza msimamo wake ikiwa kitashiriki au la uchaguzi wa duru ya pili mnamo tarehe 27.Inadaiwa kwamba kiongozi wa chama hicho Morgan Tsvangirai anashinikizwa kujiondoa kushiriki uchaguzi huo kutokana na kuenea kwa ghasia zinazohusishwa na zoezi hilo.

Wakati huo huo picha mpya zilizorekodiwa na mfanyikazi mmoja katika ubalozi wa Marekani zimeonyesha wapiganaji wa chama tawala wakiwa wamebeba fimbo na marungu wakiwasaka wafuasi wa chama cha MDC mjini Harare.

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa linatazamia kurudi tena siku ya jumatatu kwenye kikao kuijadili hali hiyo ya kisiasa nchini Zimbabwe kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais wa duru ya pili.

Baraza hilo lenye wanachama 15 litajadiliana juu ya ripoti itakayotolewa na mjumbe wake Haille Menkerios aliyeko Zimbabwe na kukutana na rais Mugabe pamoja na kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC Morgan Tsvangirai.Mjumbe huyo pia alikutana jana na rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini mjini Pretoria.

Wakati huohuo Marekani imetangaza kuunga mkono juhudi za rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini za kusimamia mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kisiasa katika mgogoro wa Zimbabwe ambayo huenda yakajumuisha suala la uwezekano wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.Jumatano iliyopita rais wa Afrika kuisni alijaribu kumshawishi rais Mugabe kufutilia mbali duru ya pili ya uchaguzi itakayofanyika tarehe 27 ili kutoa nafasi ya kufanyika mazungumzo juu ya kuundwa serikali ya Umoja wa kitaifa.