1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe ashikilia msimamo wa kutojiuzulu

Grace Kabogo
17 Novemba 2017

Rais Robert Mugabe ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutojiuzulu wadhifa wake, wakati wa mkutano kati yake na majenerali wa ngazi ya juu wa kijeshi ambao wamechukua udhibiti wa Zimbabwe.

https://p.dw.com/p/2nmZO
Rais Mugabe na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Constantino Chiwenga

Mazungumzo hayo yamefanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Harare, baada ya wanajeshi kuzuia barabara kuu, kuchukua udhibiti wa kituo cha televisheni ya taifa pamoja na kumuweka katika kizuizi cha nyumbani Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 93, pamoja na mkewe Grace na mawaziri kadhaa.

Kituo hicho cha televisheni kilimuonyesha Mugabe akiwa amevalia koti la rangi ya buluu iliyokoa pamoja na suruali ya kijivu akiwa amesimama pamoja na Mkuu wa Majeshi, Constantino Chiwenga aliyekuwa amevalia sare za kijeshi. Mugabe ambaye ameitawala Zimbabwe tangu ilivyopata uhuru wake mwaka 1980 kutoka kwa Uingereza, amekataa kuachia madaraka, baada ya kukutana pia na wajumbe kutoka Afrika Kusini.

Simbabwe Harare Mugabe mit General Chiwenga
Mugabe katika mazungumzo kuhusu mzozo wa ZimbabwePicha: Reuters/Zimpapers/J. Nyadzayo

Taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo ya kuutatua mzozo wa Zimbabwe, yanaendelea. Awali, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma aliliambia bunge la nchi yake mjini Cape Town, kwamba ni mapema mno kuchukua uamuzi thabiti kutokana na hali ya kisiasa iliyopo, ambayo muda si mrefu itajulikana wazi.

Kiongozi wa upinzani wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai amemtaka Mugabe kuondoka madarakani. Tsvangirai waziri mkuu wa zamani na mpinzani wa muda mrefu wa Mugabe amewaambia waandishi habari mjini Harare kwamba kiongozi huyo anapaswa kujiuzulu kwa maslahi ya wananchi. Amesema kipindi cha mpito kitahitajika ili kuhakikisha kuna utulivu.

Mwanasiasa mwigine wa Zimbabwe anayeheshimikwa kimataifa, Tendai Biti amesema njia inabidi ipatikane ili kudumisha utulivu. Biti aliyewahi kuwa waziri wa fedha wakati wa serikali ya muungano baada ya uchaguzi wa mwaka 2008, amesema mpango wa amani unahitajika na kwamba malalamiko yaliyosababisha hali hiyo yanapaswa kujadiliwa.

Umoja wa Afrika una imani na SADC

Umoja wa Afrika umesema utairuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa Kusini mwa Afrika-SADC, kuwa mpatanishi katika mzozo wa kisiasa wa Zimbabwe. Kamishna wa amani na usalama wa Umoja wa Afrika, Smail Chergui amesema umoja huo una matumaini kwamba hatua ya jeshi la Zimbabwe kuchukua madaraka, inaonyesha kuwa kuna juhudi za kufuata sheria, badala ya kuwepo mapinduzi. Amesema kuwa wajumbe wa SADC wamefanikiwa kukutana na Rais Mugabe na kwamba Afrika ina imani na juhudi zao.

Bonn Staatspräsident Guinea Alpha Conde
Rais wa AU, Alpha CondePicha: DW

Kwa upande wake Rais wa Umoja wa Afrika, Alpha Conde amesema umoja huo hautaruhusu mapinduzi ya kijeshi nchini Zimbabwe. Akizungumza na DW, Conde ambaye ni Rais wa Guinea, ametoa wito wa kurejeshwa kwa utawala unaotambuliwa kikatiba na ametaka katiba ya Zimbabwe iheshimiwe.

Jumuia ya kimataifa imekuwa ikiufuatilia mzozo huo kwa karibu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametoa wito wa kupatikana suluhu kwa njia ya amani nchini Zimbabwe. Msemaji wa Guterres, Stephane Dujarric amesema umoja huo una wasiwasi na kwamba hautaki kuona nchi hiyo inakosa utulivu.

Katika taarifa yake, Guterres amesema anafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea nchini Zimbabwe, na ametoa wito wa kuwepo utulivu na kusisitiza umuhimu wa kupatikana suluhisho kwa njia ya amani, ikiwemo kufanya mazungumzo. Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa ameunga mkono juhudi zinazofanywa na SADC katika kuumaliza mzozo huo.

Portugal Lissabon Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa UN, Antonio GuterresPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Govern

Ama kwa upande mwingine, viongozi wa Ujerumani wamesema wana matumaini kwamba mabadiliko yoyote yale nchini Zimbabwe yatafanyika kwa njia ya demokrasia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Rainer Breul amesema kuwa Ujerumani na washirika wake wa Umoja wa Ulaya wamewasihi viongozi wa jeshi nchini Zimbabwe kujizuia na ghasia kutokana na hali inayoendelea kwa sasa nchini humo. Ujerumani imezitaka pande zote kushirikiana ili kupata ufumbuzi kwa amani.

Kwa miaka mingi, Ujerumani na Zimbabwe zimekuwa na uhusiano mzuri na imara. Mwaka 1982 aliyekuwa Kansela, Helmut Schmidt alimpongeza Mugabe, ambaye kwa wakati huo alikuwa waziri mkuu, kwa kusaidia katika harakati za ukombozi na kuchangia kwa kiasi kikubwa nchi hiyo kujipatia uhuru wake kwa njia ya amani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman