1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muhammad Ali kuzikwa Louisville, Kentucky

5 Juni 2016

Bondia gwiji Muhammad Ali atazikwa Ijumaa, Juni10, baada ya ibada maalum ya wazi itakayofanyika katika ukumbi maalumu, ambapo rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton atakuwa miongoni mwa watakaotoa wasifu wake.

https://p.dw.com/p/1J0jx
Muhammad Ali Cassius Clay 1978 New Orleans
Picha: picture-alliance/dpa

Maisha ya bondia huyo gwiji Muhammad Ali yataombolezwa kwa msafara wa mazishi wa umma na sala maalum wiki ijayo katika mji alikozaliwa wa Louisville, jimboni Kentucky, amesema msemaji wa familia siku ya Jumamosi.

Ali, bingwa wa dunia mara tatu katika uzito wa juu na mwanaharakati aliyekuwa na mvuto mpigania haki za kiraia, ambaye umaarufu wake ulisambaa katika nyanja zote za michezo kote duniani na kumfanya kuwa alama maalum ya karne ya 20, alifariki siku ya Ijumaa (03.06.2016) akiwa na umri wa miaka 74 baada ya kupambana kwa muda mrefu na ugonjwa wa kutetemeka, Parkinson's.

Mohammed Ali aliwasha mwenge wa Olimpiki mjini Atlanta
Mohammed Ali aliwasha mwenge wa Olimpiki mjini AtlantaPicha: Getty Images

Bondia huyo aliyekuwa na mvuto, ambaye maneno yake mara nyingi aliyoyatoa kwa mashairi ya vina, yalikuwa makali kuliko makonde yake, alilazwa katika hospitali ya Arizona mapema wiki hii.

Kumbukumbu

Kuanzia viongozi wa kisiasa hadi wana michezo na wacheza sinema wa Hollywood wa kiwango cha juu, dunia ilisimama kumkumbuka "The Greatest," ambaye muda wake wa kupigana ngumu ulichukua mihula mitatu, na ambaye mapambano yake na ugonjwa baadaye katika maisha yake yaliwagusa mashabiki wake.

Baada ya ibada maalum ya mazishi ya faragha katika familia yake siku ya Alhamis, jeneza la Ali litapitishwa mitaani mjini Louisville siku ya Ijumaa, Juni 10, kabla ya kufanyika ibada maalum ya kumbukumbu katika ukumbi maalum.

Msafara utakaofuata jeneza, umeandaliwa "kuruhusu kila mmoja atakayekuwapo duniani kusema kwaheri," msemaji wa familia Bob Gunnell amewaambia waandishi habari.

Alifahamika kwa kujigamba kuwa bondia bora duniani
Alifahamika kwa kujigamba kuwa bondia bora dunianiPicha: picture-alliance/empics

Mji wa Louisville ulishusha bendera nusu mlingoti kwa heshima yake, wakati mashabiki walimiminika katika nyumba yake alikozaliwa, ambayo hivi sasa ni nyumba ya makumbusho, kutoa heshima zao na kuweka maua.

Rais Barack Obama aliongoza wasifu kwa Ali, akitoa taarifa ya binafsi ambapo alisema anazo glavu za kupigania za Ali na picha katika chumba chake maalum cha kusomea.

"Muhammad Ali alikuwa bingwa wa kweli. Bila shaka," rais wa Marekani amesema, akimsifu Ali kwa ukweli wake na kusema "Alisimama wakati ilikuwa vigumu, alisema wakati watu wengine wasingweza."

Ali asimama kidete

"Mapambano yake nje ya ulingo wa ngumi yalimgharimu ubingwa wake na nafasi yake katika jamii. Alijitengenezea maadui kushoto na kulia, yalimfanya achukiwe na karibu afugwe jela. Lakini Ali alisimama kidete," Obama alisema. "Na ushindi wake ulitusaidia kuzowea Marekani tunayoifahamu hivi leo."

Obama baadaye alimpigia simu mjane wa Ali, Lonnie, akimwambia, "Ni muhimu kiasi gani kushuhudia "bingwa" akibadilisha mzunguko wa historia."

Katika mapitio ya wasifu ambao huenda Bill Clinton atautoa, yeye pamoja na mkewe Hillary, ambaye anawania kuteuliwa na chama cha Democratic kuingia Ikulu ya White House, wamesema Ali alikuwa "mchanganyiko wa uzuri na madaha, kasi na nguvu ambazo huenda hazitawezekana kulinganiwa tena.

Muhammad Ali aliugua ugonjwa wa Parkinson's
Muhammad Ali aliugua ugonjwa wa Parkinson'sPicha: picture alliance/abaca/L. Hahn

Ali alilazwa hospitali katika eneo la Phoenix mapema wiki hii, lakini hali yake iliporomoka haraka, na familia yake ilikusanyika kando ya kitanda chake.

"Saa zake za mwisho zilikuwa pamoja na familia yake ya karibu," Gunnell amesema, akidokeza kwamba sababu rasmi ya kifo chake kuwa ni mshituko wa maambukizi kutokana na sababu zisizoeleweka za kiasili.

Ali alikuwa akiishi katika eneo la Phoenix na mkewe Lonnie. Ndoa yake ya nne, ilifanyika mwaka 1986. Ana watoto tisa, wasichana saba na wavulana wawili.

Mpiganaji huyo binafsi amepanga sehemu kubwa ya matukio ya kumbukumbu yake ya mazishi, Gunnell amesema.

Maombolezi yatakayokuwa ya dini mbali mbali yatafanyika mjini Louisville Kentuky katika kituo cha Yum, kwa mujibu wa utamaduni wa Kiislamu na chini ya uangalizi wa Imam.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid