1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musharraf aapishwa kuwa Rais kwa kipindi cha pili

Mohammed Abdul-Rahman29 Novemba 2007

Asema uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa Januari mwaka ujao

https://p.dw.com/p/CUV9
Musharraf (kushoto) katika hafla ya kujiuzulu ukuu wa majeshiPicha: AP

Kiongozi wa Pakistan Pervez Musharraf ameapishwa rasmi leo kuwa Rais kwa kipindi cha pili, lakini safari hii akiwa ni kiongozi wa taifa wa kiraia. Musharraf pamoja na hayo amelikataa kabisa shinikizo la kimataifa kumtaka aondowe sheria ya hali ya hatari. Kuapishwa kwake leo kunafuatia kujivua ukuu wa majeshi hapo jana.

Musharraf aliyechukua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi yasiomwaga damu 1999, alikula kiapo cha kuwa kiongozi mkuu wa taifa hilo la Pakistan kwa kipindi kingine cha miaka mitano, mbele ya jaji mkuu mpya Abdul Hameed Dogar Ikulu mjini Islamabad.

Kustaafu kwake jana kama mkuu wa majeshi kulitokana na mbinyo mkubwa nyumbani na nje ya nchi kumtaka amalize miaka minane ya uatawala wa kijeshi uliokumbwa na misukosuko, kabla ya uchaguzi mkuu tarehe 8 Januari mwaka ujao.

Katika hotuba yake kwa taifa Musharraf mwenye umri wa miaka 64, alisema hii ni hatua kubwa mbele katika kipindi cha mpito kuelekea demokrasia iliokamilika nchini humo. Aliahidi kuwa lolote naliwe lakini uchaguzi mkuu utafanyika kama ilivyopangwa, licha ya kitisho cha kususiwa na mawaziri wakuu wawili wa zamani Bibi Benazir Bhutto na Bw Nawaz Sharif.

Lakini kwa mara nyengine aliupuuza wito mpya wa Rais George W. Bush wa Marekani na washirika wengine wa magharibi kumtaka aondowe sheria ya hali ya hatari aliyoitangaza tarehe 3 mwezi huu wa Novemba.

Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ya kuapishawa Rais Musharraf mbali na mamia ya wageni waalikwa, ni pamoja na mkuu mpya wa majeshi Jenerali Ashfaq Kiyani.

Saa chache kabla ya kuapishwa kwake Musharraf, Rais Bush na waziri wake wa mambo ya nchi za nje Condoleezza Rice waliipongeza hatua yake ya kujiuzulu ukuu wa majeshi, lakini wakamtaka aondowe sheria ya hali ya hatari ili kuhakikisha uchaguzi ujao unakua huru na wa haki.

Musharraf alisema , „tunataka demokrasia, tunataka haki za binaadamu, tunataka uhuru wa raia-lakini yote yatapatikana kwa njia yetu sisi.“ Akipuuza kile alichokiiita“ mfumo wa demokrasia wa magharibi usioendana na ukweli na hali halisi ya Pakistan. Akaongeza „ Sisi ndiyo tunaoielewa jamii yetu na mazingira yetu vizuri zaidi kuliko mtu mwengine yeyote katika ulimwengu wa magharibi.“

Sheria ya hali ya hatari kwa upande mwengine imezusha hatua mpya ya mgogoro wa kisiasa ulioanza mwezi Machi , wakati Musharraf alipomfukuza kazi kwa mara ya kwanza jaji mkuu Ifrikhar Muhammad Chaudhry kabla ya kuondoshwa kabisa Novemba 3.

Wanasheria katika mji wa mashariki wa Lahore wamesema wataandamana leo kupinga kuapishwa Musharraf kuwa rais, sheria ya hali ya hatari na msimamo wake kuhusu mahakama. Akiwa rais wa kiraia, Musharraf atakua na madaraka ya kuifukuza serikali, lakini anatarajiwa kukabiliwa na changamoto kutoka kwa viongozi wa upinzani Bhutto na Sharif, ambao wote walirudi nyumbani karibuni kutoka uhamishoni.