1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musharraf ajiuzulu

Hamidou, Oumilkher18 Agosti 2008

Ulimwengu wasemaje baada ya Musharraf kujizulu?

https://p.dw.com/p/F0L7
Maandamano dhidi ya MusharrafPicha: AP




Maelfu kwa maelfu ya wapakistan wameteremka majiani kushangiria mara baada ya rais Pervez Musharraf kutangaza anajiuzulu,kufuatia mwaka mmoja na nusu wa maandamano dhidi ya kiongozi huyo.Wapakistan na walimwengu kwa jumla wanasemaje?



"Hata sentensi yake "nimeamua kujiuzulu" hajawahi kuimaliza, na umati ulihanikiza na kuanza kushangiria kutoka kila pembe ya Pakistan ambako watu walikusanyika majiani kusikiliza hotuba yake kwa njia ya televisheni hii leo....




Mjini Lahore,mji mkubwa wa mashariki,kitovu cha maandamano ya tangu March mwaka jana dhidi ya Musharraf,ngoma za kienyeji zilihanikiza saa kadhaa hata baada ya hotuba kumalizika,watu wakipiga makelele "Musharraf atokomee.Bwana mmoja anasema:


"Nnahisi ni vizuri kwake kujiuzulu.Watu wote wamemgeukia;viongozi wa kisiasa,wananchi ,mpaka vyombo vya habari...."


Taifa zima liko furahani" anasema kwa upande wake Saba Gul,mwanafunzi wa chuo kikuu cha Lahore.


Mjini Peshawar,mji mkubwa wa kaskazini magharibi,karibu na zoni za kikabila ambako jeshi limeanzisha hujuma dhidi ya wanamgambo wa Al Qaida na wafuasi wa Taliban,milio ya risasi imesikika leo jioni kushadidia hisia za chuki dhidi ya Musharraf.Sawa na mjini Multan,alikozaliwa waziri mkuu Yusuf Raza Gilani,waandamanaji wanaisujudia ardhi na kumshukuru Mungu.


Simu za mikono zimehanikiza,watu wanapeana mikono ya furaha.Hata hivyo kuna wengine walioingiwa na hofu,mfano wa huyu anaesema:


"Ametaka kumaliza vurugu lililotokea.Wengi tumeshtuka tuliposikia kwamba anajiuzulu.Kwa maoni yangu mie,nikiwa muandishi habari,nadhani leo ni siku ya kiza kwa historia ya miaka ijayo ya Pakistan."


Upande wa kimataifa,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na serikali ya Pakistan.Serikali kuu ya Ujerumani,imesema kupitia msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje mjini Berlin,wanataraji rais mpya wa Pakistan atachangia katika kuimarisha utulivu nchini Afghanistan na katika kupambana na ugaidi.


Uengereza imemsifu rais Pervez Musharraf,lakini imehakikisha wakati huo huo kwamba uhusiano pamoja na Pakistan hautategemea hatima ya mtu mmoja.


Na hatimae India inasema kujiuzulu Pervez Musharraf ni suala la ndani la Pakistan.