1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mustakabali wa Afghanistan kujadiliwa

4 Desemba 2014

Zaidi ya viongozi wa nchi 70 wanaokutana mjini London, wametoa ahadi ya kuendelea kushirikiana na Afghanistan, wakati ambapo Jumuiya ya NATO, ikiendelea kuviondoa vikosi vyake nchini humo

https://p.dw.com/p/1Dz6c
Baadhi ya viongozi wanaohudhuriwa mkutano wa Afghanistan
Baadhi ya viongozi wanaohudhuriwa mkutano wa AfghanistanPicha: Getty Images/AFP/O. Scarff

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na rais mpya wa Afghanistan, Ashraf Ghani wanatarajiwa kuuongoza kwa pamoja mkutano huo, utakaohudhuriwa pia na wawakilishi wa mashirika ya misaada, makundi ya haki za binaadamu na vyama vya kiraia. Lengo kuu la mkutano huo ni kuhakikisha kwamba Afghanistan inaendelea kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa katika kupambana na wapiganaji wa Taliban.

Mkutano huu wa 12 kuhusu Afghanistan, unafanyika huku kukiwa na wimbi la ghasia mpya nchini humo. Katika wiki za hivi karibuni pamekuwepo na mashambulizi yanayowalenga raia wa kigeni, wanajeshi pamoja na raia wa kawaida. Wiki iliyopita, wanajeshi wawili wa Marekani na wafanyakazi wawili wa ubalozi wa Uingereza waliuawa katika mashambulizi tofauti, huku Waafghani kadhaa wakiuawa pia na wengine walijeruhiwa.

Waafghani wengi wanaamini kuwa Taliban inautumia mwanya wa kipindi cha mpito kufanya mashambulizi hayo, wakati ambapo serikali inajipanga kujisimamia na kujiendesha yenyewe. Asilimia kubwa ya majeshi ya NATO yataondoka Afghanistan ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, huku kikosi kidogo kikiendelea kubakia nchini humo kwa ajili ya kutoa mafunzo. Vikosi vya NATO vimekuwa vikiendesha operesheni za kijeshi kwa miaka 13. Hata hivyo, wengi wana hofu kuhusu kile kitakachoweza kutokea pindi majeshi ya kimataifa yatakapoondoka.

David Cameron akiwa na Rais Ashraf Ghani
David Cameron akiwa na Rais Ashraf GhaniPicha: Reuters/O. Sobhani

Miaka 15 yahitajika kuujenga uchumi wake

Aziz Rafiee kutoka Jukwaa la Chama cha Kiraia cha Afghanistan, anasema Afghanistan inahitaji angalau muda wa miaka 15 kuujenga uchumi wake wenyewe ili iweze kujiendesha. Hata hivyo, Afghanistan imefanikiwa kupata maendeleo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, tangu jumuiya ya kimataifa ilipoingia nchini humo na miradi ya misaada, baada ya kuanguka kwa utawala wa Taliban mnamo mwaka 2001. Masoud Trashtwal, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Afghanistan anasema kuwa mkutano wa London ni fursa kubwa kwa Afghanistan.

''Wakati huu jumuiya ya kimataifa inataka ahadi maalum kutoka kwa Afghanistan katika suala la kuwaajiri watu waaminifu kwenye nafasi za serikali na kuiondoa serikali yenye rushwa. Kama serikali itashindwa kutimiza ahadi hiyo kwa jumuiya ya kimataifa kwa wakati muafaka, basi sisi tutakosa fursa zote,'' alisema Trashtwal.

Rais Ghani atakuwa akitafuta kuidhinishiwa ahadi za fedha kwa ajili ya mpango wake wa kuufanya mwaka ujao kuwa 'muongo wa mabadiliko' ambao utaimarisha serikali anayoiongoza. Hata hivyo, Rais Ghani atakuwa katika shinikizo la kuongeza juhudi zaidi katika kupambana na tatizo la rushwa, ambalo litakuwa ajenda kuu ya mkutano huo. Afghanistan bado inategemea msaada wa kigeni kwa zaidi ya asilimia 90 ya pato lake la ndani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,DW
Mhariri: Iddi Ssessanga