1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel PK

Maja Dreyer15 Januari 2008

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliarifu kuwa mwaka huu wa 2008 ni wa muhimu zaidi kuonyesha faida ya serikali ya muungano kati ya vyama vikubwa vya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/Cq2I
Kansela Angela MerkelPicha: AP
Katika hotuba yake iliyosubiriwa sana baada ya wiki ya mivutano kuzidi kati ya wanachama wa vyama vinavyounda serikali hii ya mseto, Kansela Angela Merkel alisema anaamini kuwa kazi zitakazofanywa mwaka huu zitaonyesha ikiwa serikali hii ya muungano imefanikiwa au la.


Kulingana na Kansela Merkel, malengo muhimu zaidi ni kuwa na bajeti iliyo sawa hadi mwaka wa 2011, kupunguza gharama za kazi zinazolipwa na waajiri na kuongeza fehda zinazolipwa kwa ajili ya utafiti. La muhimu zaidi lakini ni kupunguza idadi ya watu wasiokuwa na ajira ili watu wengi iwezekanavyo wanufaishe kutokana na kukua kwa uchumi.


Kansela huyu alitaja pia kuhusu mada ambayo imesababisha migogoro mingi, yaani uhalifu wa vijana. Mada hiyo inatumiwa na waziri mkuu wa mkoa wa Hessen, Roland Koch, katika kampeni yake ya uchaguzi wa mkoa utakaofanyika Jumapili ijayo. Katika suala hilo, Angela Merkel ambaye ni wa chama cha Christian Demokrats CDU alimmunga mkono mwanachama wenzake Koch katika kutaka hatua zinazochukuliwa kuwaadhibu vijana wahalifu ziwe kali zaidi, kwa mfano kuwatia gerezani vijana kwa muda mfupi kama kuwapa onyo au kuwarejesha nyumbani vijana wahalifu wa asili ya kigeni haraka zaidi.  Ni jambo la kusikitisha kuwa nusa ya vitendo vya uhalifu vinafanywa na vijana walio chini ya umri wa miaka 21, Bi Merkel alisema: "Na kwamba katika takwimu hizo za vitendo vya uhalifu kuna ishara nyingi ambazo zinaonyesha kuwa nusu ya vitendo hivi vinafanywa na vijana wa asili ya kigeni. Hakuna jibu moja tu. Kuanzia kuzuia uhalifu hadi kutoa adhabu inabidi kutumia njia hizo zote. Lakini naamini ni suala linaloweza kujadiliwa hadharani. Katika kampeni ya uchaguzi haipaswi kuwa na masuala yasiyoweza kugusiwa."


Kwa kusema hivyo, Kansela huyu alimtetea waziri mkuu wa mkoa Roland Koch kuzungumzia suala hilo katika kampeni ya uchaguzi. Koch alikuwa alikosolewa kwa sababu ya kutumia mada hiyo kujipatia kura nyingi zaidi. Bi Merkel lakini alisema pia ametambua kuwa chama cha Social Democrats SPD hakioni haja ya kubadilisha sheria kuhusu wahalifu vijana.


Kuhusu masuala ya kigeni, Kansela Merkel anataka kuendelea na sera zake. Alisema mahusiano na China ni mazuri licha ya serikali ya China kukasirika baada ya Merkel kumwalika kiongozi wa kidini wa Tibet, Dalai Lama, katika ofisi yake mjini Berlin. Merkel: "Serikali ya Chinai inajua kwamba katika masuala mengi kuna uhusiano wa kirafiki kati ya Ujerumani na China ambao haujabadilika."


Kuhusu uchumi, Bi Merkel alisisiza kuwa kodi hazitapunguzwa, kwa vile dunaini kote hakuna matumaini uchumi kuboreka zaidi. Vilevile alionya juu ya kuweka mishahara ya chini ambayo inaweza kupunguza nafasi za ajira. Serikali imeanda mswada wa kuweka sheria, lakini inabidi mswada huu urekebishwe.