1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa benki Ulaya bado kitendawili

Beate Hinrichs16 Septemba 2013

Nchi za Umoja wa Ulaya zinapendelea kuwa na chombo kimoja kinachosimamia mabenki katika umoja huo, lakini hakuna anaependa kukilipia chombo hicho.

https://p.dw.com/p/19iRt
Picha: Johannes Eisele/AFP/GettyImages

Muungano wa benki ndiyo mradi muhimu zaidi wa Umoja wa Ulaya katika miaka ya hivi karibuni, lakini itachukua muda mrefu kuufanikisha kutokana na vizingiti kadhaa vinavyoukabili. Mawaziri wa fedha wa nchi za Umoja wa Ulaya waliokutana katika mji mkuu wa lithuania Vilinius wiki iliyopita, walikuwa mbali kabisaa na muafaka juu ya kuanzishwa kwa umoja wa mabenki kuliko walivyokuwa mwaka mmoja uliyopita.

Hali katika chumba cha mkutano ilikuwa ya mawingu kama ilivyokuwa kwa hali ya hewa nje ya mkutano huo. Kwa mara nyingine tena, mvutano kati ya taasisi za Umoja wa Ulaya umekwamisha juhudi za kuanzishwa kwa muungano wa mabenki. Muungano huo ambao rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso aliuita mradi wa kifahari zaidi wa Umoja huo, ambao ulipangwa kuanza mwezi Machi mwaka huu, umegueka mhanga wa kushindwa kwa Umoja wa Ulaya kuchukua hatua.

Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso.
Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso.Picha: Reuters

Sasa kuanza mwakani
Mwaka uliyopita, viongozi wakuu wa nchi na serikali za Umoja wa Ulaya waliamua kuanzisha umoja wa mabenki mwenzi Machi mwaka huu, kwa kuweka usimamizi wa pamoja wa mabenki hayo.Lakini lengo hilo halikuweza kufikiwa kutokana na baadhi ya maswali kutoweza kujibiwa. Na sasa mjumbe wa Ujerumani katika bodi ya benki kuu ya umoja wa ulaya Jörg Asmusen alitangaza mjini Vilinius, kuwa watakuwa tayari kuanzisha "chombo cha usimamizi wa benki katika majira ya mapukutiko mwaka ujao. Ni ratiba yenye malengo makuu lakini inatekelezeka."

Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya ECB pia inahitaji kuajiri wataalamu wa fedha wapatao 1,000, watakaofanya kazi katika chombo cha usimamizi katika makao yake makuu mjini Frankfurt. Wazo la kuanzisha umoja wa mabenki lilikubaliwa hapo awali kama nyenzo ya kuzuwia migogoro huko mbeleni, lakini mataifa kadhaa yakiwemo Ujerumani na Uingereza, yana wasiwasi kuhusu namna utakavyotekelezwa kwa vitiendo.

Waziri wa fedha wa Uholanzi Jeroen Disselbloem, ambaye ndiye mwenyekiti wa kundi la mawaziri wa fedha wa umoja huo maarufu kama "Euro-Group", alisema kumekuwepo na vizingiti vya hapa na pale, na kwamba wanatarajia kuwa na mjadala mpana katika miezi michache ijayo, ambao utahitimishwa ifikapo mwezi Novemba au Desemba. Disselbloem alisisitiza kuwa siyo kwamba mpango wa kuanzisha muungano wa benki unadhoofishwa, akibainisha kuwa kuna maendeleo yaliyofikiwa, ambapo hatua ya kwanza - ambayo ni chombo cha usimamizi, SSM iliidhinishwa na bunge la Umoja wa Ulaya Alhamisi wiki iliyopita.

Nani atalipia mabenki yanayofungwa?
SSM ilipewa jukumu la kusimamia sekta ya benki katika kanda inayotumia sarafu ya euro chini ya muongozo wa benki kuu ya Umoja wa Ulaya ECB, ikilenga kuhakikisha kuwa matatizo madogo katika benki za mataifa hayakuwi na kuathiri mabenki yote. SSM itaendeshwa na benki kuu ya ulaya, lakini sasa jambo linalozua mjadala ni hatua inayofuata, ambayo ni kuundwa kwa chombo cha pamoja, kitakachosimamia kufungwa kwa mabenki yaliyofeli, ambacho kinatarajiwa kuanza kufanya kazi mwaka 2018.

Mwenyekiti wa mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya, Jeroen Dijsselbloem.
Mwenyekiti wa mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya, Jeroen Dijsselbloem.Picha: picture-alliance/dpa

Mpango wa sasa ni kwa chombo hicho kuwekwa chini ya Halmashauri ya Ulaya, lakini hilo litamaanisha upanuzi zaidi wa mamlaka ya halmashauri hiyo. Kamishna wa masoko ya fedha wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier alisema halmashauri hiyo haina nia ya kuchukua kazi hiyo, lakini ililaazimika kuchukua uongozi kutokana na haja ya kutuliza mfumo wa benki na kuyawezesha mabenki kuendelea kuwakopesha wafanyabiashara.

Hata hivyo, Jörg Asmussen alisisitiza kuwa kabla ya kuanza kuujaribisha mfumo huo kwa mabenki makubwa 130 ya Umoja wa Ulaya, laazima ibainishwe wazi kwanza, wapi zitatoka fedha za kufilisi mabenki yanayofeli. Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinavutana juu ya gharama, kwa sababu kila mmoja inataka kuepusha kugusa katika bajeti yake ya taifa.Lakini Asmussen alieleza kuwa nchi wanachama zinapaswa kulegeza misimamo yao ya sasa kwa sababu "mgogoro wa Umoja wa Ulaya umeonyesha kuwa ufilisi wa mabenki katika mataifa mbalimbali haukuratibiwa ipasavyo."

Mjumbe wa bodi ya ECB kutoka Ujerumani, Jörg Rasmussen.
Mjumbe wa bodi ya ECB kutoka Ujerumani, Jörg Rasmussen.Picha: picture-alliance/dpa

Nani anapaswa kuamua benki zipi zifungwe?
Swali linalozidi kukuna vichwa kwa sasa ni nani anaamua ni benki zipi zifilisiwe - hasa inapokuwa benki ina matawi katika mataifa mbalimbali ya Ulaya. Halmashauri ya Ulaya imejipendekeza kuwa mamlaka ya ufulisi, hatua ambayo inaungwa mkono na benki kuu ya Ulaya ECB, lakini mawaziri kadhaa wa fedha, akiwemo Wolfgang Schäuble wa Ujerumani, hawako tayari kuruhusu mamlaka hiyo kutoka mikononi mwao. Na badala yake wanataka mamlaka zao za taifa kuwa na kauli ya mwisho kuhusu hatma ya mabenki.

Mvutano mwingine uliyochangia kuchelewesha uanzishwaji wa muungano wa mabenki ulikuwa katika vifungu vya kisheria na maandishi. Lakini kwa baadhi ya wachumi na mtalaamu wa Umoja wa Ulaya, Janis Emmanouilidis, hili haliwashangazi kwa kuzingatia kuwa hali ya mambo imetulia katika kanda inayotumia sarafu ya euro ikilinganishwa na mwaka moja uliyopita.

"Hili linadhihirika hasa katika kile kinachojulikana kama ushughulikiaji wa mabenki, ambapo mapendekezo yaliyowasilishwa na halmashauri ya umoja wa Ulaya kwa baadhi ya mataifa ikiwemo Ujerumani, yanakwenda mbali mno. zimefanyika juhudi za kubuni mfumo unaosababisha mabadiliko madogo na yasiyo ya kina kama ilivyofikiriwa mwaka moja uliyopita. Tuna shinikizo dogo katika kasi na pia katika suali la umbali gani tunapaswa kwenda," anasema Emmanuoilidis kutoka shirika la ushauri la European Policy Centre.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wonfgang Schäuble.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wonfgang Schäuble.Picha: DW/B. Riegert

Schäuble ataka walipakodi wasibebeshwe mzigo
Katika kipindi cha miaka michache ijayo, muungano huo unapaswa kuwa na mtaji wake wa kiasi cha euro bilioni 60, ambazo zinapaswa kuchangiwa na benki zilizomo katika Umoja wa Ulaya. Nchini Ujerumani, wengi wanahofu kuwa jukumu la kuokoa mabenki yanayofeli kusini mwa Ulaya litabebwa na mabenki ya nchini humo kwa gharama ya wateja wao. Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble anasema Ujerumani inataka muungano wa benki uanzishwe haraka iwezekanvyo, lakini uwemo katika misingi madhubuti na masuluhisho ya busara. Waziri Schäuble anasema jambo moja linapaswa kuwekwa wazi kabisaa kwa wahusika wote ili kuyaepusha makosa ya awali.

"Wajibu na dhima laazima viwe pale fursa zilipo. Na hiyo ni kwa wamiliki wa mabenki na wenye amana, na si kwa walipa kodi. Hilo laazima liwekwe wazi. Zaidi ya hapo laazima pia kuwepo na ufafanuzi juu ya mgawanyo wa hasara inayotokana na ufilisi wa benki kati ya wamiliki na wenye amana," anasema Schäuble kutoka chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU.

Rais wa benki kuu ya Ujerumani Jens Weidermann alibainisha kuwa muungano wa mabenki hauko katika nafasi ya kutatua matatizo ya sasa ya mabenki, bali unatizamiwa kuzuia kutokea migogoro mingine huko mbeleni.

Bomu bado halijateguliwa
Kama mzaha vile, mawaziri hao wa fedha wa Umoja wa Ulaya walikutana mjini Vilinius siku moja kabla ya kumbukumbu ya miaka mitano ya kuanguka kwa benki kubwa nchini Marekan ya Lehman brothers - tukio hilo linachukuliwa kuwa ndiyo chanzo cha mgogoro wa fedha wa dunia, ambao ulisababisha migogoro ya madeni katika mataifa ya Ireland, Ugiriki, Ureno, Italia na Uhispania barani Ulaya.

Ulimwengu wa fedha bado hautabiriki, asema Janis Emmanouilidis.
Ulimwengu wa fedha bado hautabiriki, asema Janis Emmanouilidis.Picha: DW/B.Riegert

Akizingatia mambo yote yaliyoboreshwa ili kuzuwia mgogoro mwingine, mchumi Janis Emmanouilidis, anasema ingawa kumekuwepo na maboresho kadhaa yanayolenga kuzuiwa mgogoro mwingine kutokea, bado yapo mambo mengi yanayoendela kutia wasiwasi.

"Inawezekana kuwa tunarudi tulikotoka, au tuko tena katika njia ya utaratibu wa hatari. Hapo huwezi kusema kuwa bomu limeteguliwa. Swali ni iwapo tumejifunza chochote kutokana na kufilisika kwa benki ya Lehman Brothers, na wahusika wa mabenki na taasisi za fedha wanafahamu hatari zilizopo kutokana na yale ambayo hawakuyajua huko nyuma," anasema Janis Emmanouilidis.

Mwandishi: Riegert Bernd/DW/ Iddi Ismail Ssessanga/dpae, afpe, rtre
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman.