1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa Saudia watangaza usitishaji mapigano Yemen

Mohamed Dahman
19 Novemba 2016

Muungano unaongozwa na Saudi Arabia Jumamosi (19.11.2016) umetangaza usitishaji wa mapigano wa masaa 48 kwa masharti waasi wa Kishia wauzingatie na kuruhusu kufikishwa kwa misaada ya kibinadamu katika miji iliozingirwa.

https://p.dw.com/p/2Swsy
Jemen Waffenruhe
Picha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Hata hivyo dakika chache baada ya kuanza utekelezaji wake wanaharakati katika mji wa Taiz wamesema kwamba mashambulizi ya mizinga ya waasi yanaendelea katika mji huo wakati msemaji wa kijeshi anayehusiana na waasi amesema kwamba hakuna mapigano yaliyositishwa.

Kanali Sharaf Loqman msemaji huyo wa kijeshi ameliambia shirika la habari la AP kwamba hakuna mapigano yaliyositishwa katika medani yoyote ya mapambano. Amesema waasi wanaunga mkono usitishaji kamili wa uhasama lakini kiuhalisia kwa sasa pande zote ziko katika mapigano.

Shirika la habari la Saudia SPA limekuwa na taarifa kutoka kwa muungano unaogozwa na Saudi Arabia inayosema usitishaji wa mapigano utaanza kutekelezwa sasa sita mchana saa za Yemen hapo Jumamosi na kwamba usitishaji huo unaweza kuongezewa muda.Muungano huo umewaonya waasi wanaojulikana kama Wahouthi dhidi ya kujihusisha kijeshi kwa njia yoyote ile.

Usitishaji huo wa mapigano unakuja wakati vikosi vilivyo tiifu kwa serikali inayotambuliwa kimataifa inayoungwa mkono na Saudi Arabia vikisonga mbele huko Taiz mji ambao umezingirwa na waasi kwa mwaka mmoja sasa.

Dai la muungano

Jemen Ruinen in Taiz
Madhara ya mashambulizi kusini magharibi mwa mji wa Taiz.Picha: Reuters/A. Mahyoub

Muungano huo ulikuwa ukidai Wahouthi watume wawakilishi wao kukutana na kamati ya kusitisha mapigano ilioko katika mji wa kusini wa Saudi Arabia ili kuandaa mipangilio ya usalama na kijeshi kukomesha udhibiti wa waasi kwa miji kadhaa ilioko kaskazini mwa Yemen ukiwemo mji mkuu wa Sanaa.

Wakati muungano huo ukisisitiza kwamba usitishaji huo wa mapigano unakusudia kufunguwa njia ya amani haukufafanuwa iwapo inaukubali mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa ambao unamweka kando Rais Abed Rabbo Mansour Hadi na kuwapa nafasi waasi kushirikiana madaraka.

Usitishaji huu wa mapigano pia unakuja siku mbili baada ya mpango wa awali wa kusitisha mapigano chini ya usimamizi wa Marekani kwenda kombo.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ambaye amekutana na wawaklishi wa Wahouthi nchini Oman wiki hii ameweka tarehe 17 Novemba kuwa ni siku ya kuanza kwa usitishaji wa mapigano.

Mpango huo ulikataliwa mara moja na serikali ya Hadi ambayo inamshutumu Kerry kwa kufanya makubaliano ya upande mmoja.Muungano huo unaongozwa na Saudi Arabia haukutowa kauli yoyote ile kuhusu tangazo hilo la Kerry.

Maafa na madhara

Jemen Unterernährung
Mwananchi wa Yemen akikabiliwa na utapia mlo.Picha: Reuters/A. Zeyad

Mzozo nchini Yemen umeigawa nchi hiyo katika maeneo yanayohasimiana ambako huko kaskazini yakikaliwa na Washia na huko kusini yakikaliwa na Wasuni chini ya udhibiti wa muungano na Saudi Arabia.

Muungano huo uliigilia nchini Yemen hapo mwezi wa Machi mwaka 2015 kufuatia ombi la Hadi ambaye alilazimika kuikimbia nchi hiyo wakati Wahouthi walipojiunga na vikosi tiifu kwa Rasi Ali Abdullah Saleh aliyeondolewa madarakani kwa kutoka kwenye eneo lao kaskazini mwa nchi hiyo na kuuteka mji mkuu na kuanza kusonga mbele kulekea kusini mwa nchi hiyo.

Mashambulizi ya anga ya majeshi ya muungano na mapigano yanayoendelea yamesababisha vifo vya raia 4,000 na kujeruhi wengine maelfu.Mzozo huo umewapotezea maakazi watu milioni tatu na kuliweka taifa hilo la kimaskini katika ulimwengu wa Kiarabu kwenye ukingo wa baa la njaa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AP

Mhariri : Zainab Aziz