1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MUZIKI HULETA FARAJA

Christopher Buke25 Septemba 2007

Nyimbo za zamani Haziishi utamu zinaendelea kupendwa.

https://p.dw.com/p/CHjD
Chombo mojawapo chenye nyuzi kama alichokuwa akikung'uta Dk. Remmy Ongala
Chombo mojawapo chenye nyuzi kama alichokuwa akikung'uta Dk. Remmy OngalaPicha: BilderBox

“Weka Remmy Ongala!” alihanikiza kijana mmoja aliyekuwa katika baa iitwayo Masiwa Family mjini Bagamoyo ambapo kwa nasibu siku hiyo nilitoka ili kujumuika na rafiki zangu ili kutoa ushamba machoni.

Kijana huyu alitoa ombi lake mara mbili na akiisha gundua kuwa DJ kampuuza na kuweka wimbo mwingine aliinamisha kichwa chake na kuendelea ‘kupata taratibu’, kama wafanyavyo waungwana.

Badala ya kumsikiliza mteja yule DJ aliweka wimbo ambao nadhani aidha aliutaka au aliodhani unapendwa zaidi na wateja wengi. Wimbo huo ni wa 20 % uitwao Binti kimanzi. Basi ndo ukatutumbuiza si unajua tena mara “ ukitaka utamuoa eeh mtoto tulia”, na kadhalika na kadhalika.

Baadhi ya niliokuwa nao wakaonyesha hisia za kuvutiwa na wimbo huo. Mwenzangu yule aliyekuwa ameomba wimbo wa Dk. Remmy ambaye alikuwa amekaa meza ya katikati ya ukumbi wa baa ile akaendelea kuinamsiha kichwa chake. Binafsi nikadhani amekubali matokeo, kumbe bado analo.

Mara tu wimbo huo wa 20 % ulipokuwa unaishiria akapaza tena sauti yake “Tuwekee Remmy Bwana”, bahati mbaya na mara hii hakusikilizwa. Mbaya zaidi hata wimbo uliowekwa na DJ safari hii na sisi ukaanza kutuboa.

Taarabu yenyewe ikawa si taarabu maana inaimba kwa kuzorota kama vile kanda ina matatizo. Mwenzangu yule akaendelea kuinamisha kichwa mara hii akilaani kichini chini.

Mara moja nikajifunza kitu na hivyo nikawauliza rafiki zangu tuliokuwa tumekaa meza moja kama wanaweza kugundua kwa nini yule jamaa hatulii bila kuchezewa wimbo wa Dk. Remmy Ongala?

Mwenzangu mmoja aliyeonekana kuwa shapu kujibu swali langu alimwangalia kwa udadisi kisha akanijibu “ halafu jamaa mwenyewe anaonekana kachoka!”, kikafuata kicheko tena cha kuiba-iba, si unajua mambo ya baa? ili isibainike tunacheka nini.

Lakini baada ya kicheko na mimi kama paparazzi nikadadisi na kisha nikakubaliana na mada iliyokuwa imetolewa na mwenzangu na mimi. Nadhani huenda ikawa ndio sababu ya kutaka achezewe mwimbo wa Remmy Ongala.

Na kusema kweli hili ndo likaja kunikumbusha maneno aliyowahi kuniambia Dk. Remmy ongala Mwenyewe pale nilipomuuliza sababu ya nyimbo zake nyingi kuzungumzia zaidi mambo ya kawaida kabisa ambayo twakutana nayo katika maisha ya kila siku?

“ Nalikuwa natunga kwa sababu nalikuwa mi napenda sana wanyonge. Wale wa under dog. Watu wa masikini ndio nilikuwa napendelea sana kuzungumzia nyimbo zangu.

Sana nilikuwa napendelea kuzungumzia wamasikini kwa sababu mimi ni masikini pia, na masikini hakuna mtu wa kumtetea. Masikini ukiwa masikini ni nguvu zako ndo zitakufanya angalau ule. Mpaka ufanye kazi sana kwa bidii utoke jasho sana upate kula”.

Lakini kwa upande mmoja kutokana na kisa cha mwomba wimbo wa Remmy na DJ ndipo nikagundua kwa nini baadhi ya ma-DJ huwa maarufu lakini wengine wakaendelea kusota.

Wasio endelea mara nyingi hushindwa kujua vipi vionjo vya wateja wao kosa ambalo lafanywa pia na wanamuziki wengi nchini hasa wale wanaoinukia.

Wamestahiki kujiuliza swali, kwa nini nyimbo zilizotungwa zamani zingali zikipendwa mpaka leo wakati baadhi ya nyimbo zinatungwa na baada ya muda mfupi zinatoka kwenye chati, na zinasahauliwa kabisa?.

Tena nawaambia kabisa kuwa wala wasihangaike kujichubua au kujiweka heleni za almasi au kuvaa pete za vikuku vya dhahabu, wala kujiangalia kwenye vioo kama wana sura zinazovutia. Watu hawatapenda nyimbo zao kwa sababu ya uzuri au ubishoo wa wao na bahati nzuri yeye Dk. Remmy katika mmoja wa nyimbo zake aliisha sema hadharani kuwa “ sura yangu mbaya lakini roho yangu nyeupe”.

Kumbe watu wanataka nini? Wanataka ujumbe. Nyinyi siku hizi ndo mnaita meseji. Sawa nakubali. Watu wanaposikia muziki wanalinganisha na matatizo waliyokuwa nayo au raha wanazopata na kiasi fulani mirindimo katika muziki huo. huko ndiko kupendwa muziki na ukadumu.

Wanamuziki wengi hasa wale wa zamani wanalifahamu hili na kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiniambia sababu ya nyimbo zao kuvuma kwa muda mrefu. Hata Remmy mwenyewe siku moja aliniambia suala hilo.

“ Tatizo yao hawa vijana hawataki kutuambia sisi kusema nyinyi wakubwa zetu nyinyi mlianzaga namna gani? Tungekuwa tunawaeleza tulianzaga hivi na hivi basi! Mwenyewe atakuja tutamuambia ataendeleza hiyo muziki tu”, aliniambia Mzee Remmy.

Na kweli kuna siri hapo kuwa licha ya miaka mingi imepita lakini bado mtu anateremsha vitu vyake huku akidai “ Weka Remmy Ongala” na sio anasema kwa bahati mbaya anahanikiza tena “ Weka Remmy Bwana”. kwa sababu kuna kitu ndani ya mziki huo kinamkuna.

Kile ambacho sikukifahamu kwa mara moja ni mwimbo gani hasa miongoni mwa nyimbo za mkongwe huyo yule Bwana alitaka kuchezewa? Lakini kwa mantiki tuliyoongelea kuna nyimbo nyingi za Dk. Remmy ambazo zawaliwaza wale ambao siku hizi wanaitwa wasio nacho.

Miongoni mwa hizo ni ule wa BWANA MDOGO. Katika wimbo huo Dk. Remmy anamtuma Bwana mdogo (ambaye sijui ni nani) awaambie wazazi wake kijijini kuwa wasione ukimya wa Dk. Remmy wakadhani amewapuuza bali anatafuta lakini bado hajapata.

Anaendelea kulalamika katika wimbo huo kuwa hawezi kurudi nyumbani mikono mitupu asilani katika wakati ambao amepoteza miaka mingi jijini Dar es salaam akitafuta lakini hajapata. Tena anatoboa siri kuwa wazazi wake wasidhani anatumbua. Anaweka wazi kuwa wakati mwingine hata nguo hafui.

Je ni mwimbo huu yule Bwana alikuwa akiuomba? Sijui. Pengine ni ule wa MUME WANGU? Ambao Mwanamke anamlalamikia mumewe kuwa anakwenda kwenye starehe kila siku kurudi saa nane usiku.

Mwanamama anahoji kama ni starehe si waende wote? Kwani anakuwa na nini huko? Mbaya zaidi akithubutu kumuuliza mume wake anatoka wapi mumewe anamjia juu kwa kumpita mateke na magumi kwa hiyo mwana mama huyo anamkejeli mumewe kuwa “Pole pole mume wangu, haina ujanja hiyo. Haina dawa haina kinga”.

Je ni huu huyu Bwana akiuomba? Nachelea sio maana yeye alikaa peke yake pia kwenye meza pale Masiwa Family Bar. Sikuona pembeni mwake mwanamama wala mwanadada.

Kumbe ni upi? Au ni ule ambao Dk. Remmy anatoa mwito watu wajuliane hali akisema “ Jamani dunia, sote tupo safarini, tusaidiane wakati wa shida, nyumba ya jirani yako kuna msiba, wewe waweka mdundiko usiku kucha? hujui kufa wewe”, labda ni huu.

Vyovyote vile iwavyo anajua mwenyewe ni mwinbo gani alitaka, lakini kwa hisia zangu inawezekana alitaka wimbo wowote uliochezwa na mwanamuziki huyo, kama ni hivyo ni kwa nini? Labda ni kutokana na kile ambacho mwenyewe Dk. Remmy amekuwa akikitaja bayana kuwa yeye ni Sauti ya mnyonge.

Labda kwa vijana wa siku hizi au wageni ambao kwa sababu moja au nyingine mtakuwa hamumfahamu mwanamuziki huyu Dk. Remmy Ongala, ni mwanamuziki maarufu nchini Tanzania aliyevuma sana kwenye miaka ya 81, baada ya kuundwa bendi yake ya Super Matimila.

Ni mtanzania mwenye asili ya Nchi ya Jamhuri ya Congo DRC. Alizaliwa mwaka wa 1947 katika eneo la Kivu nchini DRC wakati ule ikiitwa Zaire.

Hivi sasa ameacha mziki aliokuwa akipiga anasema “ sasa hivi namwimbia Mwenyezi MUNGU”. Makazi yake ni Sinza eneo lijulikanalo kama Zinza kwa Remmy jijini Dar es salaam.

Mwenyewe Dk. Remmy hapingi wala hapigi vita muziki wa siku hizi ambao wengi mnauita mziki wa kizazi kipya. Anasema anawapongeza sana. Lakini nilipomuuliza bendi anazozihusudu anasema anaipenda Msondo Ngoma. Anasema bendi hiyo ingali kwenye mstari.

Anasema nyimbo hizi za zamani zitaendelea kupendwa tofauti na baadhi wanavyodhani kuwa zitaisha au kufa kifo cha kawaida.

“ Ile muziki haiwezi kupotea! Kama mziki wa Mbaraka Mwishehe, mbona mbaraka Mwishehe alikufa zamani na muziki mpaka sasa hivi ikipigwa sisi wote tunaipenda? Kwa sababu ile haiwezi kufa, kwa sababu tungali tupo, ile muziki yetu haitakufa mpaka sisi wazee tulishakufa.

Wakati wetu tulishakufa wote na hatuwezi kufa wote! Sasa hivi tungali tunaishi tu, kwa hiyo mziki huo utakuwa upo tu na kutakuwa tu vizazi vingine, hii sasa hivi ni wakati wa vizazi vipya lakini time nyingine itakuja muziki wetu utakuwa juu vile vile. Kuna wengine wataiga hiyo”, anasema Dk. Remmy. Namimi naogopa kupinga ubashiri wake maana siku ile pale Masiwa Familly Bar jamaa asingedai mara mbili na ushee, Niwekee Remmy!.

Ndiyo maana nilipomuuliza Dk. Remmy atoe ushauri kidogo kusudi na mimi nifanye kazi ya kuupeleka kwa waimbaji vijana alinipa kidogo na mimi sio mchoyo, huo hapo chukua.

“ Ushauri wangu nataka kuwashauri tu wana-bendi wenzangu ya kuwa kazi ya muziki ni kazi kama kazi nyingine yoyote, na waendeleze kufanya kazi yao kama kawaida na manyimbo zao ziwe za nini? za ujumbe.

Wasiende sana nje ya nchi yetu. Wasiige sana nyimbo za magharibi, waige nyimbo za kwetu tu, za kiafrika. Kama sisi masikini hatuwezi kuwa masikitu kwa muziki. Tuko masikini kwasababu ya kula ndiyo, ya pesa hatuna, lakini katika mziki wetu iwe pale pale. Ndiyo nilikuwa napenda niwaambie hata vizazi vipya wawe na hiyo kitu”.

Je kama wewe ni mwanamuziki wa kizazi kipya unakubali kuwa na hiyo kitu? Utajua mwenyewe tena mie nafunga virago vyangu na kuondoka hadi Juma lijalo. ALAMSIKI.

Mwisho.