1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kati ya Marekani na Israel wazidi.

20 Julai 2009

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa Israel haitachukua amri yoyote kuhusiana na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi.

https://p.dw.com/p/It0V
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: AP

Mvutano mpya kati ya Marekani na Israel juu ya ujenzi wa makaazi 20 katika eneo moja la mji wa Jerusalem lililonyakuliwa wakati wa vita vya mwaka 1967 huenda ukawa mbaya kati ya washirika hao wawili.

Maafisa kutoka Israel wanasema kuwa wizara ya mambo ya nje ya Marekani imemwita balozi wa Israel nchini Marekani, Michael Oren, na kumfahamisha kuwa ujenzi ulioidhinishwa mwezi huu na Isreal unastahili kusitishwa.

"Hatuwezi kukubali kuwa suala kuwa wayahudi hawatakuwa na haki ya kuishi na kununua makao popote pale katika mji wa Jersalem", alisema Netanyahu huku akiutaja Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, mji ambao hata hivyo hautambuliwi kimataifa.

Netanyahu na rais wa Marekani Barack Obama wana tofauti kutokana na wito wa rais Obama wa kuitaka Israel isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika ardhi ambayo Wapalestina wanaipigania kuwa taifa lao.

Mjumbe wa rais Obama katika mashariki ya kati, George Mitchel, ambaye atarejea eneo hilo hivi karibuni pamoja na waziri wa ulinzi nchini Israel, Ehud Barak, wamekuwa wakijaribu kupata suluhisho, likiwemo la kuzitaka nchi za kiarabu kuboresha uhusiano wao na Israel.

Akijibu matamshi ya Netanyahu, mpatanishi kutoka mamlaka ya Palestina, Saeb Erakat, alisema kuwa Netanyahu anastahili kuelewa kuwa ujenzi wamakaazi ya Wayahudi na amani ni vitu viwili ambayo haviambatani.

Israel ililiteka eneo la mashariki mwa Jerusalem na kuutangaza mji wa Jerusalem kuwa mji wake mkuu baada ya vita vya mwaka 1967. Wapalestina wanadai kuwa ujenzi wa makaazi ya ayahudui katika ardhi iliyotoweka kutawanyima haki ya kuwa na taifa lao.

Ardhi hiyo ilinunuliwa na tajiri mmoja wa Kimarekani, mwenye asili ya kiyahudi mwaka 1985, na ambaye amekuwa akifadhili ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi mashariki mwa mji wa Jerusalem.

Kituo kimoja cha runinga cha kibinafsi kilisema kuwa tajiri huyo ameanzisha mradi mpya wa ujenzi wa makaazi mapya 69 Mashariki mwa mji wa Jerusalem katika eneo la Ras al Hamud. Zaidi ya mamia ya makaazi mengine yako katika eneo hilo.

Manispaa ya mji wa Jerusalem ilisema kuwa iliidhinisha ujenzi wa makao ishirini. Manispaa hiyo ilisema kuwa ilipata ardhi hiyo kihalali, ikisema kuwa kulingana na mahakama kuu nchini Israel Wayahudi, Waislamu na Wakristo wanaweza kununua ardhi katika kila eneo la mji wa Jerusalem.

Wapalestina wamekuwa wakipinga ujezi huo, wakisema kuwa eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na kiongozi wa dini mjini Jerusalem, Haj Amin al Hessein, ambaye alienda uhamishoni mwaka 1937 na kuaga dunia mwaka 1974.

Wakati huo huo, waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, anarajiwa kuizuru Israel tarehe 27 mwezi huu kafanya mazungumzo ambayo yanatarajiwa kuangazia zaidi mipango ya kinyuklia ya Iran, pamoja na uhusiano uliopo kati ya Marekani na Israel.

Robert Gates pia atazungumzia njia za kutafuta suluhisho la mzozo kuhusu makazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mwandishi :Jason Nyakundi/RTRE

Mhariri :Othman Miraji