1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kati ya vyama vinavyounda serikali ya muungano Pakistan

Hamidou, Oumilkher21 Agosti 2008

Nawaz Sharif atishia kukitoa chama chake katika serikali ya muungano

https://p.dw.com/p/F2Eo
Viongozi wawili wakuu wa serikali ya muungano Pakistan,Nawaz Shariff (kushoto) na Asif ZardariPicha: picture-alliance/ dpa




Viongozi wa serikali ya muungano nchini Pakistan,waliomtia kishindo rais Pervez Musharraf mpaka akajiuzulu jumatatu iliyopita,wanashindwa kusawazisha hitilafu zao za maoni kuhusu nani anastahiki kua rais na pia kuhusu suala la kurejeshwa kazini majaji waliofukuzwa na Pervez Musharraf.


Viongozi wa vyama vinne vinavyounda serikali ya muungano wamekua wakikutana tangu jumanne ,lakini mazungumzo yao hayajaleta tija yoyote mpaka sasa.


Mvutano umeripuka kati yao kuhusu hatima ya majaji waliofukuzwa kazi mwaka jana na Pervez Musharraf.Waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif ametishia kukitoa  chama chake  toka serikali ya muungano ikiwa uamuzi hautafikiwa hadi kesho kuwarejesha kazini majaji hao.


Nawaz Shariff ameliambia gazeti la Wall Street Journal "majaji hao lazma warejeshwe kazini "akihoji kufukuzwa kwao kumeathiri misingi ya kidemokrasi ya nchi hiyo.


"Sio kwamba tunataka kuiangusha serikali.Lakini bila ya shaka,hatutakua na njia isipokua kukalia viti vya upande wa upinzani."Amesema Nawaz Shariff.


Chama cha PPP,kinachoongozwa na Asif Ali Zardari, aliyekua mume wa waziri mkuu wa zamani,marehemu Benazir Bhutto,kinasita sita linapohusika suala la kuwarejesha kazini majaji hao.Kinahofia pengine majaji hao wasije wakabatilisha msamaha uliotolewa kwa wanachama wao wanaotuhumiwa kuhusika na rushwa.


Viongozi wa vyama viwili vidogo katika serikali hiyo ya muungano,wanafifiisha mvutano huo ,hata hivyo wanasema wamewapatia wenzao muda wa siku tatu wasawazishe hitilafu zao za maoni.


Nawaz Shariff anadai Zardai alimuahidi hivi karibuni majaji watarejeshwa kazini,saa 24 baada ya Pervez Musharraf kutimuliwa madarakani."Tumemuunga mkoni ili Musharraf ang'olewe madarakani.Hivi sasa ni zamu yake kutuunga mkono majaji warejeshwe kazini."Amesema hayo Nawaz Shariff mbele ya ripota wa gazeti la Wall Street Journal.


Vuta nikuvute nchini Pakistan inaangaliwa kwa jicho la wasi wasi katika nchi jirani ya India.Waziri wa mambo ya nchi za nje Anand Sharma anasema:


"Tunaitakia Pakistan utulivu na amani pamoja na kuimarisha demokrasia."


Wadadisi wanahisi kujitoa chama cha Nawaz Shariff katika serikali ya muungano,hakutamaanisha kuitishwa uchaguzi wa kabla ya wakati,wakishadidia kwamba chama cha PPP,chenye wingi mkubwa bungeni,kinaweza kujipatia uungaji mkono wa kutosha kutoka vyama vyengine ili kuendelea kuwepo madarakani.


Nawaz Shariff amezidi kujipatia umaarufu tangu alipofanikiwa kumng'owa madarakani rais Musharraf na kushikilia warejeshwe kazini majaji hao.Wadadisi wanahisi pia chama cha PPP kisingependelea kwa hivyo uchaguzi uitishwe wakati huu tulio nao.

.