1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano mpya kati ya Iran na Marekani unatokota kwenye mlango bahari wa Hormuz

Admin.WagnerD29 Desemba 2011

Msafara wa meli za kivita za Marekani umepita karibu na eneo la mlango wa bahari wa Hormuz, ambalo kwa sasa linatumiwa na jeshi la Iran katika mazoezi ya kivita.

https://p.dw.com/p/13bHf
Jeshi la majini la Iran linafanya mazoezi makubwa karibu na mlango bahari wa Hormuz
Jeshi la majini la Iran linafanya mazoezi makubwa karibu na mlango bahari wa HormuzPicha: picture alliance / dpa

Maafisa wa Iran wamesema kuwa ndege zao za kijasusi zimechukua picha za msafara huo. Haya yanatokea wakati kukiwa na mvutano mpya baina ya Iran na Marekani katika eneo hilo, kufuatia kitisho cha Iran kwamba inaweza kulifunga eneo hilo muhimu katika usafirishaji mafuta iwapo itawekewa vikwazo.

Msemaji wa jeshi la Iran Mahmoud Mousavi ameliambia shirika la habari la nchi yake, IRNA, kwamba ndege zao za kijasusi zimeiona na kuipiga picha manowari kubwa ya kimarekani yenye kituo cha ndege, ikipita karibu na eneo la mazoezi ya jeshi la Iran katika mlango bahari wa Hormuz. Marekani jana ilisema kuwa msafara wa meli zake za kivita umepita katika mlango bahari huo, ambao ni njia muhimu ya meli zinazobeba mafuta kutoka nchi za Ghuba.

Huu unaonekana kuwa mvutano mpya baina ya Iran na Marekani, kufuatia kauli ya maafisa wakuu wa Iran mapema wiki hii kuwa nchi hiyo ingeweza kuifunga kirahisi njia hiyo iwapo nchi za magharibi zitatekeleza vikwazo zaidi kwa nchi hiyo. Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani amesema hatua hiyo ya Iran haiwezi kuvumiliwa. Balozi wa zamani wa Marekani kwenye umoja wa mataifa John Bolton ameliambia shirika la habari la Fox kwamba Iran ikijaribu kufunga njia hiyo itakuwa ikijiangamiza yenyewe.

Mlango bahari wa Hormuz ni njia muhimu ya meli zinazobeba mafuta kutoka nchi za Ghuba
Mlango bahari wa Hormuz ni njia muhimu ya meli zinazobeba mafuta kutoka nchi za GhubaPicha: picture-alliance/dpa

Mwanajeshi Mstaafu wa Marekani mwenye cheo cha Jenerali James Marks amesema kwa muda mrefu Marekani imeweka kikosi kikubwa kabisa cha jeshi lake la baharini karibu na mlango bahari wa Hormuz kwa makusudi ya kuhakikisha usalama wa meli za kubeba mafuta. Jenerali huyo amesema suala la kufungwa kwa njia hiyo limefikiriwa zamani sana, na mazoezi ya kukabiliana na hali yoyote yamefanywa mara elfu kadhaa.

Licha ya hayo lakini, Iran ambayo tayari inakabiliwa na vikwazo vya kimataifa kutokana na mpango wake wa silaha za nyuklia, imesisitiza iko tayari kuifunga njia hiyo iwapo itashambuliwa, au uchumi wake kuhujumiwa. Kufungwa kwa njia hiyo kunaweza kusababisha mtafaruku katika soko la mafuta ulimwenguni, na kuumiza zaidi uchumi wa dunia ambao tayari unachechemea.

Jeshi la baharini la Marekani limejihami kuhakikisha usafiri wa meli za mafuta kutoka Ghuba.
Jeshi la baharini la Marekani limejihami kuhakikisha usafiri wa meli za mafuta kutoka Ghuba.Picha: U.S. Marine Corps

Jeshi la Iran liko kati mazoezi makali ya siku kumi linayoyafanya mashariki mwa mlango bahari wa Hormuz, ambayo yanaripotiwa kujumuisha utegaji wa miripuko baharini, na matumizi ya ndege zisizo na rubani. Hadi sasa vitisho kati ya nchi hizo mbili vimeishia katika utupianaji maneno na kutunishiana misuli kupitia mazoezi ya kivita, lakini wachambuzi wana wasi wasi kwamba kichocheo kidogo kinaweza kuwasha moto kati ya nchi hizo mahasimu wa muda mrefu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu