1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa Iran na nchi za Magharibi washika kasi

8 Februari 2010

Iran yasema kesho Jumanne inaanza kurutubisha asilimia 20 ya madini ya Uranium huku nchi za Magharibi zikikusanya mawazo kuhusu kuiwekea vikwazo zaidi

https://p.dw.com/p/LvrF
Shughuli za Urutubishaji zitafanyika katika kinu cha NatanzPicha: picture-alliance/ dpa
Marekani na Ufaransa zimesema zitatia msukumo wa kupitishwa vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kuhusiana na mpango wake wa kinuklia.kwa upande mwingine Iran imeliarifu rasmi shirika la kimataifa la kudhibiti technologia ya Nuklia IAEA kuhusu mpango wake wa kutaka kurutubisha madini ya Uranium ya kiwango cha juu.Hatua hiyo imetajwa na nchi za magharibi kama ni kitendo cha uchokozi. Mjumbe wa Iran katika shirika la kimataifa la kudhibiti technologia ya Nuklia la IAEA Ali Asghar Soltanien akizungumza kutoka mjini Vienna na kituo cha televisheni cha kiarabu kinachomilikiwa na serikali cha Al-Alam amesema ameiwasilisha rasmi barua ya Iran kuhusu shughuli za kurutubisha madini ya Uranium ya kiwango cha asilimia 20.
Ali Asghar Soltanieh
Mjumbe wa Iran katika shirika la IAEA Ali Asghar Soltanieh amewasilisha rasmi barua ya Iran kuhusu shughuli za kurutubisha madini ya UraniumPicha: AP
Hatua hiyo ya leo imekuja baada ya hapo jana mkuu wa shirika la nguvu za Atomiki la Iran Ali Akbar Salehi kutangaza kwamba Tehran itaanza kurutubisha madini yake ya Uranium kufikia asilimia 20 kuanzia kesho jumanne na kwamba shirika la IAEA litaarifiwa kuhusiana na uamuzi huo kaböla haujatekelezwa.Na yote hayo yamefuatia ruhusa iliyotolewa na rais Mahmoud Ahmedinejad aliposema ''Tuliwapa kipindi cha miwezi miwili hadi mitatu kukubaliana na mpango wetu.Wakaanza njama mpya na sasa nampa ruhusa Dr Salehi kuanza shughuli za urutubishaji wa asilimia 20 ya Uranium.Mlango wa mazungumzo bado upo wazi'' Tangazo hilo limezusha kishindo katika ulimwengu wa nchi za magharibi kutokana na hofu kwamba Iran sasa inaelekea kweli katika utengenezaji wa silaha za Kinuklia.Leo Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates amefanya mazungumzo nchini Ufaransa na mwenzake Herve Morin na kusema kwamba vikwazo vipya ndio njia pekee iliyosalia kuitia adabu nchi hiyo ya Iran.Tamko ambalo limetilia mkazo kile alichokisema jana kwamba, ''Ikiwa jumuiya ya kimataifa itasimama pamoja kushirikiana na kuishinikiza serikali ya Iran isalimu amri naamini bado kishindo na vikwazo vina nafasi ya kuweza kufanya kazi'' Gates amesema mjini Paris leo kwamba anakwenda mbio kutia msukumo wa kupitishwa vikwazo vingine vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kutokana na mpango wake huo wa Kinuklia.Gates pia amekutana na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernerd Kuochner na rais Nicholas Sarkozy kuzungumzia suala hilo hilo la Iran.Ujerumani leo imeitaja hatua ya Iran kama ishara nyingie kwamba Iran haitaki ushirikiano na jumuiya ya kimataifa na kuionya tena nchi hiyo kwamba ijitaarishe kuwekewa vikwazo vipya.Sauti kama hizo zimesikika pia kutoka London ambako waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown kupitia msemaji wake amefahamisha kwamba hatua ya Iran inaichochea kuwekewa vikwazo vikali zaidi na jumuiya ya kimataifa.
UN-Sicherheitsrat berät in Kenia über Sudan
Jumuiya ya kimataifa yatia kishindo Iran iwekewe vikwazo zaidiPicha: AP
Urussi mshirika wa karibu wa Iran imerudia msimamo wake wa kuitaka Iran isafirishe madini yake ya Uranium katika nchi za nje kwa ajili ya kurutubishwa kama ilivyoamrishwa katika mpango wa Umoja wa Mataifa. Mkuu wa masauala ya Atomiki wa Iran Ali Salehi amesema katu Iran haitopeleka madini yake hayo kurutubishwa nje bali kesho jumanne inaanza rasmi kuyarutubisha katika kinu chake cha Nantaz mahala ambako imekuwa ikifanyia shughuli zake nyeti za Atomiki kwa miaka kadhaa.Aidha kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA mkuu huyo wa shughuli za Atmoki nchini Iran amewaalika pia waangalizi kutoka shirika la IAEA kutembelea kinu hicho cha Nantaz kujionea kitakachofanyika. Salehi pia amefahamisha kuwa Tehran itasimamisha mpango wake wa kurutubisha madini ya Uranium ya kiwango cha juu pale itakapokamilisha pamoja na nchi za magharibi mazungumzo ya muda mrefu kuhusu mpango uliopendekezwa na Umoja wa Mataifa . Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE Mhariri Abdul-Rahman.