1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa Kisiasa wachukua sura mpya Kenya

9 Januari 2008

---

https://p.dw.com/p/Cmmi

NAIROBI

Wafuasi wa upinzani nchini Kenya kwa mara nyingine wamezusha ghasia katika mji wa Kisumu baada ya rais Mwai Kibaki kutangaza baraza jipya la mawaziri.Rais Kibaki ameitangaza serikali yake ikiwa ni siku tisa baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi uliogubikwa na shakashaka nyingi kutoka ndani na nje ya Kenya.Taarifa ya chama cha upinzani cha ODM imesema hawaitambui serikali ya Kibaki na tangazo hilo sio halali kisheria.

William Ruto ambaye ni miongoni mwa vigogo wa juu katika chama cha ODM akizungumza na Redio Dw hapo jana juu ya hatua ya Kibaki alisema rais Kibaki anajihadaa na inabidi asubiri matokeo ya ukaidi wake.

Lakini waziri wa sheria katika serikali ya Mwai Kibaki Martha Karua ametetea hatua ya rais kibaki akisema ametekeleza wajibu wake kwa mujibu wa katiba na sheria ya Kenya.

Miongoni mwa walioteuliwa katika serikali hiyo ni pamoja na kiongozi wa chama cha ODM Kenya Bwana Kalonzo Musyoka ambaye amepewa wadhifa wa Makamu wa Rais, kiongozi wa chama cha Kanu Uhuru Kenyatta ndio waziri wa serikali za mitaa huku wizara ya fedha ikichukuliwa na Amos Kimunya.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa nje na ndani ya Kenya wanasema hatua ya Rais Kibaki itazidisha mvutano na kuzifanya juhudi za upatanishi za rais John Kufour wa Ghana kuwa ngumu zaidi.Bwana Odinga amekataa kufanya mazungumzo yoyote na rais Kibaki bila ya kusimamiwa na mpatanishi wa kimataifa.Na sasa hali ya kisiasa inaashiria kuwa ngumu zaidi kutokana na ziara ya 24 ya rais Kufour.