1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi zafarakana kuhusiana na Syria

Oumilkheir Hamidou
5 Oktoba 2016

Vikosi vya serikali ya Syria vinaendelea kusonga mbele Aleppo katika wakati ambapo mvutano wa kidiplomasia unapamba moto kati ya Moscow na Washington inayosema inazingatia"njia za kidiplomasia na kijeshi."

https://p.dw.com/p/2Qswh
Syrien Regierungstruppen rücken weiter auf Aleppo vor
Picha: Getty Images/AFP/T. Mohammed

 "Wakuu wa taasisi zinazohusika na masuala ya usalama na siasa ya nje wanakutana kuzungumzia hatua "za kidiplomasia,kijeshi,kijasusi na kiuchumi" kabla ya kukutana na rais Barack Obama na kumkabidhi hatua hizo-wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema huku ikishadidia umuhimu wa kupatikana ufumbuzi wa kisiasa.

Nchini Syria kwenyewe,wanamgambo wanaoelemea upande wa serikali wanaendelea kusonga mbele katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi ya mji wa kaskazini-Aleppo."Wanaelekea katika eneo la kati la mji huo" amesema hayo mkurugenzi wa shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam nchini Syria,Rami Abdel Rahmane. Lengo lao ni kuiteka mitaa ya karibu na mpaka wa magharibi ya Aleppo ili kuwazingira waasi kusini mashariki ya Aleppo.

Hujuma dhidi ya Aleppo zilizozoanza septemba 22 na vikosi vya serikali vikisaidiwa na Urusi ndio sababu iliyotajwa na Marekani inayounga mkono makundi ya upinzani,ili kuhalalisha uamuzi wa kusistisha mazungumzo pamoja na Urusi kuhusu Syria.

Moscow imetuma mtambo ziada wa  makombora ya kinga ya angani

Wakaazi wa Aleppo wayahama maskani yao
Wakaazi wa Aleppo wayahama maskani yaoPicha: Getty Images/AFP/T. Mohammed

Moscow imesema imesikitishwa na uamuzi huo hata hivyo imeelezea matumaini yake kuona "busara ya kisiasa" inatawala mjini Washington."Uamuzi wa Marekani haumaanishi kwamba Urusi itaachana na mipango yake ya kusaidia jeshi la wanaanga la Syria katika kupambana na magaidi" msemaji wa ikulu ya Urusi-Kremlin Dmitri Peskov amesema.

Wakati huo huo wizara ya ulinzi ya Urusi imetangaza kutuma  mtambo wa makombora ya kinga ya angani chapa S-300  katika mji wa mwambao wa Tartus,kaskazini magharibi ya Syria.

Kwa kupelekwa mfumo huo wa kinga ya makombora S-300,yakichanganyika na yale ya kimambo leo ya S-400 yaliyopelekwa Novemba mwaka jana,Urusi itakuwa inadhamini anga ya Syria kutoka vituo viwili muhimu- mji wa bandari waTartus na ule wa Hmeimim katika mkoa wa Lattakia .

Dazeni wauliwa karibu na mpoaka wa Uturuki

Hujuma za ndege za Uturuki kaskazini mwa Syria
Hujuma za ndege za Uturuki kaskazini mwa SyriaPicha: picture-alliance/abaca/AA/R. Korkulutas

Wakati huo huo shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam linasema shambulio la angani dhidi ya kijiji cha wakurd kinachodhibitiwa na wanamgambo wa dola la kiislam IS karibu na mpaka wa kaskazini mwa Syria limepelekea watu kadhaa kuuwawa na dazeni kujeruhiwa . Itafaa kusema hapa kwamba katika eneo hilo,jeshi la Uturuki sawa na  muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani wanaendeleza mashambulio dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislam.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuiters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo