1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwai KIbaki na Raila Odinga wakubali kuunda serikali ya mseto

29 Februari 2008
https://p.dw.com/p/DFfv

NAIROBI:

Rais wa Kenya Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wametia saini makubaliano ya kugawana madaraka na hivyo kumaliza mzozo wa kisiasa uliozuka baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais mwezi Desemba mwaka 2007.Mahasimu hao wawili wamekubali kuunda serikali ya mseto kati ya chama tawala cha hivi sasa na upande wa upinzani.Hafla ya kutiwa saini makubaliano hayo,ilishuhudiwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika,Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na msuluhishi mkuu wa mzozo huo,aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.

Kuambatana na mapatano yaliyotiwa saini,kiongozi wa upinzani Raila Odinga atashika wadhifa mpya wa waziri mkuu na atakuwa na mamlaka ya kuratibu na kusimamia serikali.Zaidi ya watu 1,500 wameuawa na 600,000 wengine wamepoteza makaazi yao katika machafuko yaliyozuka kufuatia uchaguzi wa Desemba mwaka jana.