1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwana wa Gadaffi ahotubia taifa

Martin,Prema/ZPR/RTRE/AFP21 Februari 2011

Milio ya risasi imesikika mapema leo hii katikati ya mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa mara ya kwanza, tangu maandamano dhidi ya serikali kuanza nchini humo.

https://p.dw.com/p/R2fA
epa02586762 Libyan leader Muammar Gaddafi delivers a speech at a foundation stone laying ceremony of the Al Ahly Club Tripoli, in Tripoli, Libya, 16 February 2011. According to news reports early 16 February, at least 38 people were injured when police clashed with hundreds of demonstrators in the Libyan city of Benghazi overnight. EPA/SABRI ELMHEDWI
Kiongozi wa Libya, Muammar GaddafiPicha: picture-alliance/dpa

Mashahidi na ripota wa shirika la habari la AFP wamesema, milio ya risasi ilizidi kusikika kufuatia hotuba iliyotolewa katika televisheni na Saif al-Islam Gaddafi.

Katika hotuba hiyo, mwana wa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, ameahidi mpango wa mageuzi na amesema, Baraza Kuu la Umma litakutana hii leo kujadili ajenda ya mageuzi dhahiri. Vile vile,serikali itatoa nyongeza ya mishahara.

Saif al-Islam Gaddafi, son of Libyan President Muammar Gaddafi speaks during a gathering in Tripoli, Libya, 24 July 2008. Libya and Italy will soon seal a deal worth 'billions' to compensate for the European country's three-decade colonial rule, Libyan leader Muammar Gaddafi's son said. EPA/SABRI ELMHEDWI +++(c) dpa - Bildfunk+++
Saif al-Islam GaddafiPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo, alionya dhidi ya hatari ya nchi hiyo kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na nchi hiyo kugawika. Amekiri kuwa polisi na wanajeshi walifanya makosa walipokabiliana na waandamanaji. Lakini amepuuza ripoti kuwa mamia ya watu wameuawa.

Kwa mujibu wa makundi ya haki za binaadamu, mapamabano ya hivi karibuni nchini humo, yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

Hiyo jana mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walikutana mjini Brussels Ubeligiji, kujadili msimamo wa kuchukuliwa na umoja huo, kuhusu maandamano ya kudai mageuzi ya kidemokrasia, yaliyoibuka katika Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton ameeleza wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa idadi ya waandamanaji wanaouawa kuanzia eneo la Ghuba hadi Afrika Kaskazini. Umoja wa Ulaya unahimiza uvumilivu na kukomeshwa matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji.