1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanaharakati wa haki za binaadam auliwa Kongo Kinshasa

Oumilkher Hamidou4 Juni 2010

Jumuia ya kimataifa na mashirika yanayopigania haki za binaadam ulimwenguni yanaishinikiza serikali ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo uchunguze kwa kina kisa cha kuuliwa Floribert Chebeya

https://p.dw.com/p/NiIi
Mwanaharakati wa haki za binaadam Floribert ChebeyaPicha: picture-alliance/ dpa/dpaweb

Jumuiya ya kimataifa na mashirika yanayopigania haki za binaadam wamelaani vikali kisa cha kuuliwa mwenyekiti wa shirika la "La Voix des Sans Voix"-Sauti ya wasiokua na sauti", katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban ki-Moon amesema amefadhaishwa mno na ripoti za kuuliwa Floribert Chebeya na kuhimiza uchunguzi wa kina ufanywe haraka kuhusu kisa hicho.

Akizungumzia ahadi zilizotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban ki-Moon ameshadidia umuhimu wa kuchunguzwa visa vyote vya mauaji kama hayo kama alivyosema" kwa kina, kwa njia ya uwazi na huru na kwa kuheshimu misingi inayofuatwa katika nchi inayoheshimu sheria."

Mwito wa kufanywa uchunguzi wa kina umetolewa pia na Umoja wa Ulaya ambao, mwakilishi wake mkuu anayeshughulikia masuala ya nchi za nje bibi Catherine Ashton amesema ameingiwa na wasiwasi kuhusiana na hali jumla ya wapigania haki za binaadamu katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Mashirika yanayopigania haki za binaadam katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo , barani Afrika na ulimwenguni kwa jumla yamelaani mauaji hayo.

Makamo mwenyekiti wa jumuiya ya haki za binaadam barani Afrika Brahima Koné anasema

"Tunataka jumuiya ya kimataifa iwajibike zaidi katika kisa hiki kwa sababu mtindo huu umekuwa ukiendelea - kila mara wanaharakati wa haki za binaadam wanashambuliwa na wanauliwa na wanaofanya maovu hayo wanaendelea na visa vyao bila ya kuadhibiwa."

Maiti ya mwenyekiti wa shirika la "La Voix des Sans Voix", Sauti ya wasiokua na Sauti-Floribert Chebeya, mwenye umri wa miaka 47 imegunduliwa Jumatano asubuhi ndani ya gari yake, katika njia inayooelekea Bas-Congo-magharibi ya Kinshasa.

Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binaadam , Chebeya aliitwa hapo awali katika ofisi kuu ya polisi ambako alikua akutane na jenerali John Numbi.

Na dereva wake pia, Fidele Bazana, hajulikani aliko. Wanaharakati wa haki za binaadam wanahofia na yeye pia ameuliwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp,Reuters

Imepitiwa na: Josephat Charo