1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamke akamatwa mauaji ya waziri Burundi

Sekione Kitojo
2 Januari 2017

Polisi nchini Burundi wanasema wamemkamata mwanamke mmoja wakimtuhumu kuhusika na mauaji ya Waziri wa Mazingira, Emmanuel Niyokuru, mwishoni mwa wiki, ingawa haifahamiki ikiwa yeye ndiye muuaji ama la.

https://p.dw.com/p/2V8eY
Burundi Gewalt ARCHIVBILD
Picha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Polisi inasema mwanamke aliyekamatwa alikuwa na waziri huyo kwenye gari wakati wa mauaji. 

Dakika chache baada ya usiku wa manane wa siku ya Mwaka Mpya, mshambuliaji alimpiga risasi na kumuua Waziri Niyokuru, wakati waziri huyo akielekea nyumbani kwake. 

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi, Pierre Nkurukiye, watu wengine wanne wamekamatwa, akiwemo mmiliki wa baa ambayo waziri huyo alikuwa akiitembelea mara kwa mara na walinzi wake wawili. 

Kwengineko nchini Burundi, polisi inasema watu saba walijeruhiwa kufuatia mashambulizi ya bomu la kurushwa kwa mkono katika kanisa moja siku ya mkesha wa Mwaka Mpya. 

Taifa hilo la Afrika ya kati limekuwa likishuhudia kipindi kirefu cha ghasia za kisiasa tangu mwaka 2015, ambapo hadi sasa watu 500  wameuwawa na wengine 300,000 wameyakimbia makaazi yao tangu Rais Pierre Nkurunziza kutangaza, kuwania na kushinda muhula wa tatu, licha ya kuzuiwa na katiba ambayo inaweka ukomo wa vipindi viwili.