1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamuziki Mashuhuri Lucky Dube auawa kwa kupigwa risasi

Jane Nyingi19 Oktoba 2007

Mwanamuziki mashuhuri wa miondoko ya Reggae duniani Lucky Dube ameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi katika jaribio la kupora gari lake mjini Johannesburg Afrika kusini.

https://p.dw.com/p/C7rn
Lucky Dube
Lucky DubePicha: picture-alliance/ dpa - Bildfunk

Lucky Dube wa umri wa miaka 43 alipigwa risasi na kuawa mbele ya watoto wake wawili katika eneo Rosettenville mjini Johannesberg. Msemaji wa polisi Cheryl Engelbrecht amesema mwanamuziki huyo mashuhuri alikuwa akimshusha mwanawe kutoka kwenye gari na kukabiliwa na watu waliokuwa wanaelekea kumpora gari lake.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Africa kusini polisi wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta washukiwa watatu wanaodaiwa kuhusika katika shambulizi hilo.Watoto wake wangali katika hali ya mshtuko kuweza kuwapa polisi taarifa itakayowawezesha kuwasaka kwa haraka washukiwa hao.

Mwanamuziki Mzwakhe Mbuli ambaye alikuwa mtu kwanza kufika katika eneo la shambulizi hilo alikuwa mchache wa maneno japo alisema secta ya muziki imepokonywa mwanamuziki mashuhuri.

Marehemu Lucky Dube ambaye ametoa kiasi cha santuri 20 katika zaidi ya miongo miwili ambayo amekuwepo kwenye muziki pia amepokea zaidi ya tuzo 20 kitaifa na kimataifa. Mwanamuziki huyo mashuhuri amezuru mataifa kadhaa ya bara Ulaya na Africa kwa tamasha kubwa za muziki ambazo huvutia idadi kubwa ya watu.

Santuri yake ya kwanza aliyotoa mwaka 1984 Rastas Never Die ilipigwa marufuku nchini Afrika kusini na utawala uliokuwepo wa ubaguzi wa rangi. Kwa mujibu wa mtandao wake unaofahamika kama Dubes, mwanamuziki huyo amerejea nyumbani baada ya ziara ya kupiga muziki ya mwezi mzima nchini Marekani.

Wakati wa maisha yake aliweza kupiga muziki sehemu mbalimbali duniani na kushirikiana na wanamuziki maarufu kama vile Sinead O‘ Oonnor, peter Gabriel na Sting miongoni mwa wanamuziki wengine.

Mauji ya Lucky Dube ni moja kati ya mauji ya watu maarufu nchini Africa Kusini nchi ambayo inatajwa kuwa inakiwango kikubwa cha mauji Duniani.Visa vya ubakaji,oporaji magari na mashambulizi ya iana mbalimbali yadaiwa ni ya juu,huku visa hivyo vikiendelea kushamiri licha ya juhudi zinazofanywa na serikali ya afrika kusini kuimarisha usalama.