Mwanamuziki Whitney Houston afariki
15 Februari 2012Habari za kifo cha nyota huyo zimekuja wakati ulimwengu wa muziki ukijiandaa kwa sherehe za tuzo ya Grammy leo Jumapili, na pia saa chache kabla ya tafrija ya chakula kwenye hotel ambapo marehemu Whitney Houston amepatwa na mauti.
Afisa wake wa habari Kristen Foster ambaye alikuwa wa kwanza kutangaza kifo hicho hakuelezea chanzo cha kifo chake. Hata hivyo katika miaka ya hivi Karibuni mwanamuziki huyo amekuwa akisumbuliwa na athari za matumizi ya madawa ya kulevya.
Whitney Houston alijipatia Umaarufu mkubwa katika miaka ya 1980 na 1990, kwa nyimbo zilizovuma kama ''How will I Know'', ''Saving all my Love for You'' na ''I will always Love You''. Alishiriki pia katika uwanja wa uigizaji na kuwa katika filamu mashuhuri ya ''Bodyguard''
Wakati wa umaarufu wake Whitney Houston alishinda tuzo sita za Grammy. Magwiji wa muziki wametoa rambi rambi zao kupitia mitandao ya kijamii, wakimueleza Bi Houston kama mtu ambaye hatasahaulika katika fani ya Muziki.
Kufuatia kifo hicho Sekione Kitoji wa DW alizungumza na mwanamuziki maarufu kutoka Tanzania Waziri Ali ambae alieleza kusikitishwa kwake.
Mwandishi Daniel Gakuba/RTRE
Mhariri Amina Abubakar