1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanariadha Mo Farah aendelea na mazoezi Kenya

27 Januari 2014

Bingwa mara mbili wa dhahabu katika Olimpiki, na ambaye pia ni bingwa wa ulimwengu katika mbio za mita 10,000 na 5,000 Muingereza Mo Farah yuko nchini Kenya lakini siyo kwa mapumziko au kujivinjari tu…hapana.

https://p.dw.com/p/1AxjI
Leichtathletik WM Moskau Mo Farah
Picha: Reuters

Mo Farah atakuwa nchini humo kwa kipindi cha wiki nne, ili kufanya mazoezi makali katika maeneo ya nyanda za juu ya Bonde la Ufa kabla ya mbio za marathon za jijini London mnamo mwezi Aprili, ambazo zitakuwa zake za kwanza kabisa katika taaluma yake ya riadha.

Mwanariadha huyo mzaliwa wa Somalia, atafanya mazoezi yake katika eneo la Iten, ambako amejiunga na wanariadha wengine sita wa Uingereza ambao waliwasili nchini humo mapema mwezi huu kujiandaa kwa Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayoandaliwa mjini Glasgow mwezi Agosti. Wanariadha hao wanaishi katika kambi ya mazoezi ya nyanda za juu inayomilikiwa na mzaliwa wa Kenya aliyewahi kuweka rekodi ya ulimwengu ya mbio za half marathon, Lorna Kiplagat. Mji wa Iten ni nyumbani kwa wanariadha maarufu wa marathon nchini Kenya ikiwa ni pamoja na Wilson Kipsang, ambaye ndiye anayeshikilia rekodi ya sasa ulimwenguni kwa upande wa wanaume.

Na wakati Farah na wenzake wakiendelea kuipasha misuli moto, naye gwiji wa Ethiopia Kenenisa Bekele tayari ana rekodi mbili za ulimwengu, lakini anasema anaimezea mate rekodi nyingine ya tatu: ambayo mara hii ni ya mbio za marathon.

Bekele atazitimka mbio za marathon za mjini Paris mnamo Aprili 6, ikiwa ni wiki moja tu, kabla ya hasimu wake wa uwanjani Mo Farah wa Uingereua kujitosa barabarani kwa mara ya kwanza katika mbio za marathon. Wote wawili watalenga kufuata nyayo za Mfalme wa Ethiopia Haile Gebreselassie na wengine waliofanikiwa kujipa changamoto ya kushiriki mbio za marathon

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman