1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

ICC: Pande zinazozozana nchini Sudan zafanya uhalifu Darfur

Tatu Karema
30 Januari 2024

Mwendesha mashtaka wa Mahakama ya ICC Karim Khan, ameliambia Baraza la Usalama la UN kuwa amebaini kuna sababu za kimsingi kuamini kwamba jeshi la Sudan na jeshi pinzani la RSF yanafanya uhalifu Magharibi mwa Darfur

https://p.dw.com/p/4bpAZ
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya ICC Karim Khan, akizungumza katika hafla ya Mamlaka Maalum ya Amani ya Colombia (JEP) wakati wa ziara ya mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, huko Bogota, Colombia, Juni 06, 2023
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya ICC - Karim KhanPicha: Chepa Beltran/LongVisual via ZUMA Press/picture alliance

Khan ambaye hivi karibuni alizuru nchi jirani ya Chad ambako maelfu ya watu kutoka Darfur wamepewa hifadhi, ameonya kwamba wale aliokutana nao katika kambi za wakimbizi wanahofia kwamba Darfur itageuka kuwa kile wanachokiita "ukatili uliosahaulika."

Khan ameihimiza serikali ya Sudan kuwapa maafisa wake wa upelelezi visa za kuingia nchini humo na kuyashughulikia maombi 35 ya msaada.

Khan ameliambia Baraza hilo la Usalama kwamba ilishangaza kutembelea kambi tofauti za wakimbizi nchini Chad ambazo watu waliopitia migogoro ya Darfur kutoka mwaka 2003 walimwambia moja kwa moja kwamba kile kinachotokea leo "ni hali mbaya zaidi kuwahi kutokea''.

Soma pia:Sudan yaahidi ushirikiano na mahakama ya ICC

Kiongozi huyo wa mashtaka wa ICC, ameongeza kuwa wakimbizi hao wanalishukuru sana baraza hilo kwa kuwapigania huku akisema kwamba watu hao wanataka haki na wanaiona mahakama hiyo ya ICC kama chombo muhimu sana cha kuhakikisha kwamba hawajasahaulika.

HukoDarfur, Khan ameonya kwamba ulimwengu unakabiliwa na kile alichokiita ukweli wa kutisha usioepukika unaohusiana na mzozo wa awali.

Jumuiya ya kimataifa yachangia hali ya kutojali sheria

Khan amesema kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuchukuwa hatua kuhusu waranti zilizotolewa na majaji huru wa mahakama ya ICC kumechangia mazingira ya kutojali sheria na kuzuka kwa vurugu zilizoanza tangu mwezi Aprili na zinazoendelea hadi leo.

Darfur, Sudan | Wasudani wanaokimbia mapigano wakiingia Chad
Watu wanakimbia mapigano Darfur Magharibi wakivuka kuvuka mpaka na kuingia Chad.Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

Katika hatua nyingine, balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Al-Harith Mohamed amepinga matamshi hayo ya Khan na kusema kuwa serikali imeshirikiana na ofisi ya mwendesha mashtaka huyo wa ICCna inasubiri afanye ziara nchini humo.

Mohammed ameishtumu mahakama ya ICC kwa kutozingatia "ushiriki wake wa kimkakati na hali halisi ya utendaji katika eneo hilo.

Soma pia: Kesi ya uhalifu wa kivita Darfur yaanza kusikilizwa ICC

Mohamed amekiita kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF) ''wanamgambo'' na kukishtumu kwa kufanya mashambulio makubwa ya kimfumo ambayo yanalenga kile alichokiita "kulazimisha safisha safisha ya kikabila'' ya jamii ya kabila la Masalit katika eneo la Darfur.

Soma pia: Sudan na makundi ya Darfur yakubaliana kuwapeleka watuhumiwa ICC

Balozi huyo ameongezea kuwa jukumu sasa ni la kiongozi huyo wa mashtaka wa mahakama ya ICC  kuamua ikiwa hali hiyo ni sawa na mauaji ya kimbari.

Mzozo wa wakimbizi wa Sudan