1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenye uraia wa Norway atangazwa waziri mkuu wa Somalia

Mohammed Khelef
23 Februari 2017

Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia amemteuwa mwasiasa asiye na uzoefu kuwa waziri mkuu wake, muda mchache kabla hajaelekea Saudi Arabia kwa ziara yake ya kwanza ughaibuni tangu aapishwe.

https://p.dw.com/p/2Y7i0
Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo
Picha: Getty Images/AFP/M. Haji Abdinur

Hassan Ali Khaire, Msomali mwenye uraia pia wa Norway, alikuwa mkuu wa shirika la nishati la Uingereza, Soma Oil, kabla ya uteuzi wake wa leo (Februari 23).

Mohamed aliyeapishwa siku ya Jumatano, mwenyewe ana uraia pia wa Marekani. Alichaguliwa mapema mwezi huu ikiwa sehemu ya hatua za kuelekea kwenye uundwaji wa serikali ya kwanza kamili baada ya robo karne nzuri. 

Rais huyo mpya ameapa kulifanya suala la usalama kuwa kipaumbele kwenye nchi ambayo bado kundi la kigaidi la al-Shabaab linaendelea kufanya mashambulizi kwenye mji mkuu, Mogadishu, na maeneo mengine. Siku ya Jumapili, bomu lililotegwa kwenye gari liliuwa watu 34.

Mapema wiki hii, al-Shabaab iliupinga uchaguzi uliomuweka madarakani Mohamed wakimuita yeye "kafiri", huku wakiapa kuendelea na mapigano.

Pia kuna wapiganaji wanaojinasibisha na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) ndani ya ardhi ya Somalia.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba