1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti wa kampeni ya Trump ajiuzulu

19 Agosti 2016

Mwenyekiti wa kampeni za mgombea wa Republican nchini Marekani Donald Trump, amejiuzulu baada ya ufichuzi kuhusiana na kazi za mwenyekiti huyo Paul Manfort nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/1Jlv1
USA Cleveland Paul Manafort Campaign Manager Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Rourke

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa baada ya kuwasili Louisiana kujionea uharibifu uliosababishwa na mafuriko jimboni humo, Trump alisema Manafort alijitolea kuachia nafasi yake mapema Ijumaa, na kumtaja kuwa "mweledi wa ukweli."

"Nimefurahishwa kabisaa na kazi yake kubwa katika kusadia kutufikisha tulipofikia leo, na hususan kazi yake kutuongoza kupita katika mchakato wa kupata wajumbe wa kutuunga mkono katika mkutano mkuu wa chama," alisema Trump.

Kujiuzulu kwa Manafort kumekuja siku moja baada ya shirika la habari la Associated Press kuripoti kuwa barua pepe za siri kutoka kampuni ya Manafort zilikinzana na madai kwamba hakuwahi kufanya ushawishi kwa niaba ya wanasiasa wa Ukraine nchini Marekani.

USA Donald Trump und Paul Manafort
Donald Trump akiwa na Paul Manafort waakti wa mkutano mkuu wa chama cha Republican mjini Cleveland Julai 21.Picha: Reuters/R. Wilking

Ushawishi kwa niaba ya wanasiasa wa Ukraine

Mawasiliano ya barua pepe kati ya naibu wa Manafort, Rick Gates, ambaye pia ni mashauri wa Trump, na kampuni ya ushawishi ya Mercury LLC, yanaonyesha kuwa kampuni ya Manafort ilipanga operesheni za siri za ushawishi kwa niaba ya chama kilichokuwa kinatawala nchini Ukraine wakati huo.

Juhudi zilihusisha siyo tu mawasiliano na wabunge, lakini pia majaribio ya kubadili maoni ya umma nchini Marekani na kukusanya taarifa za kiintelijensia kuhusu juhudi kinzani za ushawishi nchini Marekani.

Manafort na Gates hawakuwahi kujisajili kama mawakala wa kigeni kwa kazi yao kama inavyotakiwa chini ya sheria ya Marekani.

Wachunguzi Ukraine wambana Manafort

Siku ya Ijumaa wachunguzi wa kupambana na rushwa nchini Ukraine wametoa nakala za leja zilizoandikwa kwa mkono zikiainisha uwezekano wa malipo ya fedha taslimu kutoka kwa wanasiasa wa Ukraine kwenda kwa Manafort zinazozidi dola za milioni 12.

USA Cleveland Stephen K. Bannon
Mtendaji Mkuu mpya wa kampeni za Trump Stephen K. Bannon.Picha: Getty Images/K. Irwin

Taarifa za malipo zilizoainishwa katika leja hiyo zilianza kuripotiwa na gazeti la New York Times. Lakini Manafort anakanusha kuwahi kupokea malipo hayo.

Mapema wiki hii, Trump alimteua afisa mtenadaji mpya na meneja wa kampeni zake, kufuatia makosa ya mfululizo ambayo yalipelekea bilionea huyo kutoka New York kukwea nyuma ya mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton katika uchunguzi wa maoni ya umma kitaifa na katika majimbo yenye umuhimu mkubwa.

Meneja mpya wa kampeni za Trump, Kellyanne Conway, aliwaelezea Manafort na Gates kama sehemu ya watu wanne wa juu katika muundo mpya wa operesheni ya Trump, pamoja naye na Mtendaji Mkuu Stephen Bannon.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ap.

Mhairiri: Josephat Charo