1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwili wa Mandela wawekwa katika jengo la serikali

11 Desemba 2013

Jeneza lililochukua mwili wa Nelson Mandela lilipitishwa katika mitaa ya mjini Pretoria nchini Afrika kusini hadi katika jengo la Umoja, jengo ambalo ni makao makuu ya serikali.

https://p.dw.com/p/1AXCM
Nelason Mandela Abschied 11.12.2013
Mwili wa Mandela ukichukuliwa na wanajeshiPicha: Reuters

Kwa muda wa siku tatu wananchi wa Afrika kusini watapata fursa ya kuuona mwili wa kiongozi wao huyo aliyejitolea maisha yake kwa ajili ya kuwakomboa Waafrika kusini.

Viongozi kutoka mataifa ya kigeni walioko hivi sasa nchini Afrika kusini kwa ajili ya tukio la kumbukumbu ya Nelson Mandela pamoja na wana familia wamekuwa wa kwanza kuweza kuuona mwili wa Mandela katika jeneza. Umma umeanza kuruhusiwa kuingia katika jengo hilo kuanzia mchana wa leo(11.12.2013).

Picture-Teaser Nelson Mandela
Hayati Nelson MandelaPicha: picture-alliance/dpa

Jeneza litafunguliwa na uso wa Mandela utaonekana , licha ya kuwa ni kupitia kioo ambacho kitauhifadhi mwili wake.

Ulinzi waimarishwa

Kabla ya gari lililochukua mwili wa Mandela kuwasili, eneo lenye safu ya viti vilivyopangwa nusu duara mbele ya jengo hilo la serikali , eneo la uwanja ambalo limepewa jina la Nelson Mandela , lilikuwa na kelele za helikopta zilizokuwa zikizunguka angani.

Hali ya ukimywa ilitawala katika eneo hilo mara baada ya jeneza lililouchukua mwili wa Mandela lilipowasili na jeneza hilo lilichukuliwa hadi katika eneo maalum lililoinuliwa kiasi ya mita saba na wanajeshi nane waliovalia nguo za rangi ya zambarau wakiongozwa na kasisi wa jeshi wakiwakilisha vikosi mbali mbali vya majeshi na polisi.

Bendi ya jeshi ilikuwa ikipiga wimbo wa taifa , wakati polisi kadha pamoja na wanajeshi wakiwa wamesimama wakitoa heshima zao wakati jeneza lililokuwa limefunikwa bendera ya Afrika kusini likiingizwa katika jengo hilo ambalo ni makao makuu ya serikali.

Mjukuu wa Mandela , Mandla Mandela , aliongoza kundi dogo la waombolezaji waliovalia nguo nyeusi ambao walitembea kuzunguka jeneza. Ndugu wengine katika familia ya Mandela pia walihudhuria.

"Ni kitu cha kushangaza kufikiria kuwa miaka 19 iliyopita alitawazwa kuwa rais katika jengo hilo, na sasa amelala hapa," amesema Paul Letageng mmoja wa wafanyakazi katika ofisi za serikali kwa hisia kali.

Stimmen und Reaktionen zum Tod Nelson Mandelas
Ban Ki-moonPicha: Reuters/Mark Garten

Watoa rambirambi zao

Wakati wa tukio la kumbukumbu ya Mandela hapo jana viongozi kadha walitoa maelezo yenye hisia kali kuhusiana na yale Mandela aliyoyasimamia na kuyatenda katika uhai wake. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema Mandela alikuwa mwalimu wetu mkuu.

"Nelson Mandela alikuwa zaidi ya kiongozi shujaa katika wakati wetu huu. Alikuwa mwalimu mkuu. Ametufundisha kwa mifano."

Mamia ya Waafrika kusini walijipanga katika sehemu ya njia iliyotumika kuchukua mwili wa Mandela kutoka katika eneo la kuhifadhia maiti hospitalini hadi katika jengo hilo la serikali.

Mandla Mandela
Mandla MandelaPicha: picture-alliance/dpa

Mwili wa Mandela utakuwa unapelekwa katika hospitali ya jeshi hadi katika jengo hilo ambalo ni makao makuu ya serikali , hatua itakayochukua kiasi ya saa moja kila siku. Siku ya Alhamis na Ijumaa wananchi wataruhusiwa kutoa heshima zao kuanzia saa mbili asubuhi saa za Afrika kusini hadi saa tisa na nusu jioni.

mazishi ya kitaifa yatafanyika siku ya Jumapili katika kijiji cha asili anakotoka Mandela cha Qunu ambapo watu wapatao 15,000 watahudhuria.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae

Mhariri: Yusuf Saumu