1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwito kufanywa uchunguzi huru kuhusu Kenya

8 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D4Cx

WASHINGTON:

Uchunguzi huru wa machafuko yaliyozuka kufuatia uchaguzi wa rais nchini Kenya,huenda ukasaidia kuzuia umwagaji zaidi wa damu amesema mwanadiplomasia mwandamizi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani anaeshughulikia masuala ya Bara Afrika.Naibu Waziri wa Nje Jendayi Frazer amesema,Washington inachunguza hatua gani zichukuliwe kuhusu wale waliochochea machafuko nchini Kenya kufuatia kuchaguliwa tena kwa Rais Mwai Kibaki Desemba 27-uchaguzi uliozusha mabishano.

Hapo awali,maafisa mjini Nairobi walisema,Marekani imewazuia Wakenya 10 kuingia Marekani wakishukiwa kuhusika na machafuko ya nchini Kenya.Lakini Wizara ya Nje mjini Washington imesema,barua zimetumwa kwa Wakenya 8 wanaoshukiwa kuunga mkono au kuchochea machafuko.Washukiwa hao wameonywa kuwa huenda wakazuiliwa kuingia Marekani.

Zaidi ya watu 1,000 wameuawa na kama 300,000 wengine wamepoteza makazi yao katika machafuko ya nchini Kenya.Aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan anaongoza majadiliano ya upatanisho kati ya serikali na upande wa upinzani mjini Nairobi.Wakati huo huo,nchini Marekani siku ya Alkhamisi Baraza la Wawakilishi lilipiga kura 405-1 kumuhimiza Rais George W.Bush kuzuia kuipa Kenya misaada isiyohusika na huduma za kiutu mpaka pande hasimu zitakaposuluhisha mzozo wao kwa njia ya amani.