1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwito kuzingatia hofu za Afrika

P.Martin28 Septemba 2007

Maafisa waandalizi wa Benki ya Dunia wamepeleka ombi kwa Umoja wa Ulaya kurefusha muda wa makubaliano kadhaa ya biashara huru.Makubaliano hayo pamoja na nchi za Kiafrika,yanamalizika mwisho wa mwaka.

https://p.dw.com/p/CH7W

Kamishna wa Biashara wa Umoja wa Ulaya,Peter Mandelson mara kwa mara amezionya nchi za ACP yaani za bara Afrika,eneo la Karibea na Pasifiki-bidhaa zinazotoka nchi hizo zitatozwa ushuru mkubwa na Umoja wa Ulaya ikiwa hazitotia saini Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi(EPAs) ifikapo Desemba 31.

Ijapokuwa wanauchumi katika Benki ya Dunia yenye nchi wanachama 185 wanaunga mkono juhudi za kuimarisha biashara kati ya Ulaya na Afrika, wataalamu hao wamesema,muda zaidi unahitajiwa kujadili makubaliano yaliyopendekezwa na Umoja wa Ulaya kuhusika na kufunguliwa kwa masoko ya nchi za ACP.

Baadhi ya wanauchumi hao wanasema,nchi za Kiafrika zisishinikizwe na Umoja wa Ulaya kukubali haraka,masharti yanayohusika na uwekezaji na hata masuala ya ushindani katika makubaliano hayo ya biashara.Kwa maoni ya Benki ya Dunia,masuala yanayozusha wasiwasi barani Afrika yanapaswa kuzingatiwa kwa dhati na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.

Desemba 31 ikikaribia,wanadiplomasia wa Kiafrika wamesema,labda upo uwezekano wa kukamilisha makubaliano yaliyofanyiwa marekebisho kadhaa. Makubaliano hayo yahusike na biashara ya bidhaa huku masuala mengine ya ubishi yakiwekwa hadi baadae.

Hata hivyo wanadiplomasia wa nchi za Kiafrika wanasema,serikali zao na Umoja wa Ulaya zinatofautiana katika masuala muhimu yanayohusika na biashara ya bidhaa.Nchi za Kiafrika zimependekeza kuwa na kipindi cha mpito cha hadi miaka 25,ambapo nchi hizo zitalazimika kupunguza ushuru unaotozwa kwa bidhaa zinazotoka Ulaya. Lakini bidhaa nyingi hazitotozwa ushuru wo wote. Juu ya hivyo,baadhi ya maafisa katika Umoja wa Ulaya wanaamini miaka 25 ni kipindi kirefu mno.

Kwa upande mwingine,wanaharakati wanaopambana na umasikini wameeleza vipi sekta ya kilimo barani Afrika inavyoweza kuathiriwa na mmiminiko wa bidhaa za Ulaya zisizotozwa ushuru.Rais wa Shirikisho la Wakulima nchini Burkina Faso,bwana Bassiaka Dao amesema,Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi yatahatarisha uwezo wa nchi hiyo kulisha umma wake.Akaongezea kuwa sekta ya mazao ya maziwa nchini Burkina Faso,imeshaathirika. Sababu ni kwamba unga wa maziwa kutoka Ulaya ambao hulipiwa ruzuku na serikali za nchi hizo,ni rahisi kuliko maziwa yanayotoka kwa wakulima wa Burkina Faso.

Hata nchini Ghana,wakulima wanaofuga kuku wameonya kuwa watafilisika ikiwa serikali yao itatia saini Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi.Kwani katika mwaka 2004 nchi za Ulaya ziliuza zaidi ya tani 40,000 za kuku nchini Ghana na idadi hiyo bila shaka itaongezeka katika miaka ijayo.